Mkurugenzi Mipango Sera na utafiti Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Iliyasa Pakacha Haji akizungumza na wanachama wa klabu za skuli za kupiga vita dawa za kulevya wakati akifungua mafunzo kwa wanafunzi hao yaliyofanyika skuli ya Tumekuja Mjini Unguja.
Mwalimu kutoka Skuli ya faraja sheha Ngwali akiwasilisha muongozo wa klabu za skuli za kupiga vita dawa za kulevya katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanachama wa klabu hizo juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya.
Afisa kinga ,tiba na marekebisho ya tabia kutoka mamlaka ya kuudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Ali Yusuf Ali akiwasilisha mada ya matumizi ya dawa za kulevya na afya ya akili kwa wanachama wa klabu za skuli za kupiga vita dawa za kulevya huko skuli ya Tumekuja Mjini Unguja.
…………………………
Na Rahma Khamis- Maelezo 7/3/20/20
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Dad Shajak amesema Serikali imeanzisha Klabu za kupiga vita dawa za kulevya ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya utumiaji wa dawa ya kulenya Nchini.
Akifungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo wanachama wa klabu hizo huko Skuli ya Tumekuja Wilaya ya Mjini kwa niaba ya Katibu huyo Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Iliyasa Pakacha Haji amesema kuwa ipo haja ya kuweka mikakati imara ili kujikinga na janga hilo Nchini ikiwemo uwepo wa klabu hizo maskulini.
“Tunatarajia mafunzo haya yatawajengea uelewa wa athari za dawa hizo na uwezo wa kujitambua, uzalendo na kujiamini pamoja na kuwapa hisia za kuzichukia dawa hizo”alisema Mkurugenzi Pakacha.
Amesema elimu inayotolewa kwa klabu hizo itasaidia kutoa uwelewa juu ya dhana nzima ya dawa za kulevya na kuweza kujitambua sambamba na kuwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri kwa wengine juu ya madhara ya matumizi ya dawa hizo.
Amefahamisha kuwa vijana ndio wahanga wakubwa wa janga hilo wakiwemo wanafunzi wa sekondari hivyo Serikali imeamua kuweka klabu hizo maskulini ili waweze kupata elimu juu ya athari ya madawa hayo na kuweza kujikinga.
“Changamoto za dawa za kulevya ni janga la Dunia na waathirika zaidi ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa na kuwafanya vijana wetu kuwa hawana la kufanya kutokana na kuathirika na dawa hizi,” alifafanua Mkurugenzi Pakacha.
Ameongeza kuwa dawa za kulevya zinaleta athari nyingi nchini ikiwemo mmomonyoko wa maadili na kukwamisha juhudi za kuuinua Uchumi wa nchi kwani vijana hushindwa kujiajiri na kuajirika kwa kujihusisha na matumizi ya dawa hizo.
Mapema alifahamisha kuwa lengo la Serikali kuanzisha klabu hizo ni pamoja na kuchangia jitihada za Wizara ya elimu katika kuwajenga na kuwakuza wanafunzi kimaadili kwa kuwashirikisha katika mapambano hayo na kuwa jasiri kukataa kuuza au kutumia pamoja na kutoa taarifa za dawa hizo katika vyombo vya sheria.
Akiwasilisha Mada ya Matumizi ya madawa ya kulevya na Afya ya Akili kwa wanachama hao Afisa Kinga, Tiba na Marekebisho ya Tabia kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Ali Yussuf Ali amesema endapo mtu atatumia dawa za kulevya moja kwa moja huathiri ubongo wake ambapo athari nyengine hujitokeza baadae.
Amesema dawa hizo zinapoingia katika mwili wa binaadamu hubadilisha hisia,mwenendo na tabia ya mtumiaji jambo ambalo humfanya mtumiaji kufanya chochote hata kama kipo nje ya maadili.
Nao wanafunzi walioshiriki katika mafunzo hayo wamesema wamefurahi kupata elimu hiyo kwani wameweza kufahamu namna gani watajikinga na kuwalinda wengine na madawa hayo.
Hata hivyo wameahidi kuitumia vyema fursa ya kuanzisha kwa klabu hizo ambazo zinaenda kusaidia kusambaza elimu ya kuudhibiti matumizi ya dawa za kulevya maskulini na katika jamii kwa ujumla.
Hata hivyo waliwashauri wananchama wenzao kutumia vipaji vyao katika kutoa elimu Kwa jamii juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kuchora picha, kutunga mashairi , insha pamoja na makala mbalimbali zenye kuonesha athari za dawa hizo .
Jumla ya Skuli 10 zimechaguliwa kuunda klabu hizo ambapo katika mafunzo hayo skuli tano zimeshiriki kutoka Mjini Magharibi ikiwemo Dk. Ali Muhammed Shein, Mpendae ,Fraja, Jang’ombe na Kwamtipura.