VICTOR MASANGU BAGAMOYO
Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatarijia muda wowote kuwasha baadhi ya pampu ambazo zilikuwa zimezimwa kutokana na kukabiliwa na changamoto ya maji kujaa tope katika baadhi ya maeneo kwenye mtambo wa Ruvu chini uliopo Wilaya ya Bagamoyo.
Hayo yamebainishwa na Kaumu Mkurugenzi wa Dawasa Kiula Kingu wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara kwa ajili ya kugagua na kujionea mtambo wa Ruvu chini.
Kadhalika amebainisha kwamba kutokana na hali hiyo wamelazimika kutumia zaidi ya mapipa makubwa 97 ya lita 200 kwa siku kwa ajili ya kusafishia maji hayo yaweze kuwa safi na salama kwa wananchi.
“Kwa kweli maji yapo ya kutosha lakini changamoto kubwa ni machujio yaliyopo katika mtambo wa ruvu juu kujaa na matope mengi hivyo kusababisha hata maji kubadilika rangi yanakuwa kama vile ya udongo “,alifafanua Kiula.
Kadhalika alifanua kwamba hali ya kuwepo kwa maji mengi ni kutokana na uharibifu wa mazingira na kupelekea kujaa matope katika chujio.
Pia alifafanua kuwa kuwepo kwa tope kunapelekea kwa kiasi kikubwa kupungua kwa uzalishaji wa maji katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na Pwani.
“Kwa hiyo tuliomba masaa 36 kwa wananchi wetu lakini lengo kubwa lilikuwa ni kwa ajili ya kufanya marekebisho katika baadhi ya machujio yetu ya maji,”alibainisha Kiula.
Alisema kwamba kwa sasa mafundi wapo kazini kwa ajili ya kuhakikisha wanarekebisha katika maeneo ambayo yalikuwa yamejaa tope ili huduma ya maji iweze kurudi kwa wananchi muda wowote kuanzia leo.
Alisema kwamba baada ya kufanyika kwa matengenezo hayo wananchi watarajie kupata maji ya kutosha ambayo pia yatakuwa katika kiwango cha usafi.
Katika hatua nyingine Kingu alisema kwamba mtambo wa ruvu chini unazalisha maji kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kiwango cha asilimia 75 huku akisema kwa sasa kiwango kimeshuka kwa asilimia 20 kutokana na changamoto hiyo ya tope.
Hivi karibuni Dawasa walitoa tangazo la kukosekana kwa huduma ya kukata maji kwa kuzima kwa pampu na kukosekana na huduma ya maji kwa kipindi cha zaidi ya masaa 36.