Mwenyekiti Serikali za Mitaa wa Yombo – Kiwalani Bw. Muslim Dada akizungumza na Wazee wa Mtaa huo katika Mkutano uliofanyika tarehe 4/3/2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, ambaye ni Polisi Kata ya Kiwalani, Meshack Salum akizungumza na wazee wa mtaa Yombo Kiwalani katika mkutano uliofanyika tarehe 4/3/2024 Jijini Dar es Salaam
Mhazini wa Mzee Mtaa wa Yombo Kiwalani Festo Kabakaki akisoma risali katika mkutano wa Wazee uliofanyika tarehe 4/3/2024 Jijini Dar es Salaam.
Mhazini wa Mzee Mtaa wa Yombo Kiwalani Festo Kabakaki (kushoto) akimkabidhi risali Mwenyekiti Serikali za Mitaa wa Yombo – Kiwalani Bw. Muslim Dada.
Baadhi wazee Mtaa wa Yombo Kiwalani wakiwa katika Mkutano na Mwenyekiti wa Mitaa wa Yombo – Kiwalani Bw. Muslim Dada.
Mwenyekiti wa Mitaa wa Yombo – Kiwalani Bw. Muslim Dada akitoa Zawadi ya Sukari kwa wazee walioshiriki mkutano wa mwaka katika Mtaa huo.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wazee nchini wametakiwa kuwa karibu na vijana katika kuhakikisha wanatoa elimu ya uzalendo ikiwemo kufanya kazi kwa bidii jambo ambalo litasaidia kutokomeza vikundi vya uhalifu katika jamii.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Wazee wa Mtaa wa Yombo – Kiwalani, Polisi Kata ya Kiwalani, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Meshack Salum, alisema kuwa wapo baadhi ya wazee wamejikita katika shughuli za maendeleo, huku wakisahau kutoa elimu ya malezi kwa watoto wao pamoja na wajukuu.
A/Insp Salum alisema kuwa ni muhimu wazee kuwaelimisha vijana namna ya kuishi katika jamii ili waweze kufikia malengo na kuliongoza Taifa.
“Mtusaidie hawa vijana wengine ni watoto wenu au wajukuu muwaelimishe maana ya maisha, muwafundishe kufanya kazi na wawe na heshima pamoja na kuachana na makundi ambayo rafiki katika jamii” amesema A/Insp Salum.
Mwenyekiti Serikali za Mitaa wa Yombo – Kiwalani Bw. Muslim Dada, alisisitiza umuhimu kuwa kuwajali wazee katika kutatua changamoto zao, kwani Wazee ni Hazina ya Taifa hivyo ni wajibu wa kila kiongozi kuwapenda pamoja na kusimamia haki zao.
Bw. Dada alisema kuwa wazee wanamchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kushauri na kutoa maongozo kulingana na mazingira.
“Mkutano huu ni sehemu ya kuwajali wazee katika kuwasimamia na kuhakikisha haki zao zinapatikana, tumewasikiliza zao pamoja na kujadiliana namna bora ya kupata majibu rafiki ambayo yataleta ahueni kwao” alisema Bw. Dada.
Alisema kuwa wataendelea kushikamana kuwa na umoja muda wote kwa kushirikiana na wazee ili kuondoa changamoto zilizopo na kudumisha aman.
Bw. Mjumbe wa Serikali za Mtaa wa Yombo Philipo Mulashan, amesema wakati umefika kwa serikali kutoa elimu kwa jamii hasa kundi la vijana ili waweze kukabiliana na changamoto zilizopo katika jamii.
Nao baadhi ya Wazee wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali katika nyanja mbalimbali za kuleta Maendeleo kwa Taifa.
Mhazini wa Mzee Mtaa wa Yombo Kiwalani Festo Kabakaki amempongeza Mwenyekiti wa Mtaa wa Yombo kwa kujitoa kwa hali na mali katika kuwatambua wazee na kuwajali kwa kuwasaidia kutatua changamoto.
“Sisi wazee wa mtaa wa Yombo tumeguswa na uwezo wako wa kuongoza bila kuitaji malipo yoyote pamoja kuwaelimisha wazazi kuwapeleka watoto Shule na kudhibiti utolo kwa wanafunzi* alisema Mzee Kabakaki.
Katika mkutano huo wazee zaidi ya 500 walishiriki na kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu upatikanaji wa huduma muhimu pamoja na kupewa Zawadi ya Sukari kutoka kwa Mwenyekiti Serikali za Mitaa wa Yombo – Kiwalani Bw. Muslim Dada.