Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimefanikiwa kutatua hoja 21 za Muungano kati ya 25 zilizokuwepo awali.
Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo amesema hayo katika Kikao cha Mawaziri wa SJMT na SMZ cha
kujadili Masuala ya Muungano kilichofanyika Nyamanzi, Zanzibar leo Machi 05, 2024
Amesema kuwa tangu mchakato wa kutatua changamoto hizo ulipoanza, hadi sasa zimebaki hoja nne za Muungano ambazo Serikali zote mbili zinaendelea kuzitafutia ufumbuzi.
Dkt. Jafo ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa kikao hicho amesema viongozi wa pande zote mbili za Muungano wamekaa pamoja kujadili hoja hizo nne za Muungano zilizobaki na kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Amezitaja hoja nne zilizobaki kuwa ni pamoja na Suala la Sukari, Usajili wa Vyombo vya Moto, Bodi ya Pamoja na Mgawanyo wa Mapato ya iliyokuwa Sarafu ya pamoja ya Afrika Mashariki.
Kutokana na mafanikio, Dk. Jafo amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutatua hoja zilizobaki.
“Niwapongeze pia Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wataalamu mbalimbali kutoka Serikali za pande zote za Muungano kwani wamefanya kazi kubwa ya kuchakata changamoto zilizokuwepo hadi kufikia mafanikio haya,“ amesema Dkt. Jafo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili ya Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kuzungumzia hoja mbalimbali zinazokabili utendaji wa shughuli za SJMT na SMZ.
Amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umedumu kwa muda mrefu kutokana viongozi wa pande zote mbili za Muungano kukaa pamoja na kujadili changamoto zinazojitokeza kwa uwazi na kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja.
Akitolea mfano wa mafanikio ya Muungano huu, Mhe. Hamza amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayoundwa na nchi nane inaendelea kudumu kutokana na uzoefu unaopatikana Tanzania na hivyo jumuiya hiyo kuendelea kukua.
Ameongeza kuwa hoja nyingi zimeshatatuliwa hivyo mkutano huo unatoa matumaini makubwa kupatikana kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili pamoja na kuendelea kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao unatimiza miaka 60 ifikapo Aprili 26, 2024.