Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imepokea vifaa vyenye thamani yaTsh. 242,000,000 kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani USAID kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyikia Makao ya TAWIRI, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWIRI Dkt. David Manyanza ameishukuru USAID kutoa vifaa ambavyo ni muhimu katika tafiti za wanyamapori hususan sensa ya wanyamapori ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili hadi mitatu.
“Kama alivyowahi kusema Hayati Rais. Ali Hassan Mwinyi, mali bila daktari hupotea bila habari hivyo hatuna budi kuidadi wanyamapori ili kuwa na uhifadhi endelevu wa wanyamapori hapa chini “ameeleza Dkt. Manyanza.
Dkt. Manyanza amesema vifaa hivyo vina mchango mkubwa kwenye sekta ya Maliasili kwani tafiti za TAWIRI zinasaidia kuzishauri mamlaka za uhifadhi, “nitoe wito kwa wadau kujitokeza kushirikiana na TAWIRI ili kuwezesha tafiti za wanyamapori kwa ustawi wa uhifadhi na kukuza utalii ” ameeleza Dkt. Manyanza.
Kiongozi wa Idara ya mazingira na usimamizi wa Maliasili kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID), Nathan Sage, amesema kwa miaka 60 sasa, USAID imekuwa ikishirikiana Tanzania kuhifadhi bioanuwai ikizingatiwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za kibaolojia ikiwemo maliasili ya Wanyamapori ambao wana thamani kubwa ya kitamaduni, kiuchumi na kielimu.
Aidha, Bw. Sage amesema katika kuendeleza ushirikiano huo, USAID imetoa vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni 242 kwa TAWIRI ili kuimarisha uhifadhi kwa kuwezesha matumizi ya teknolojia kurahisisha tafiti za wanyamapori
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TAWIRI Dkt. Eblate Mjingo amesema Jukumu kuu la TAWIRI ni kufanya tafiti za wanyamapori ambapo ameishukuru USAID kutoa vifaa ambavyo ni Kamera za kufunga kwenye ndege wakati wa kuidadi wanyamapori, Mikanda ya visukuma mawimbi ya Tembo (GPS Collars) na Vifaa vya Majira nukta (_Location GPS_)
“Utafiti ni gharama, unahitaji vifaa na teknolojia, hivyo vifaa hivi tulivyopokea vinakwenda kusaidia sana hususani kwenye sensa ya wanyamapori.