Na Sophia Kingimali.
Taasisi ya Vertex imempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitahada zake za kuhakikisha tiba utalii inakuwa na kuitangaza nchi Duniani kote kwa kuboresha miundombinu na vitendea kazi katika hospitali nchini.
Pongezi hizo amezitoa leo Machi 4,2024 Jijini Dar es Salaam Meneja mkuu wa Veltex Herbert Swai wakati akizungumza na waandishi wa habari na wagonjwa kutoka nchi ya Morroco waliopata matibabu nchini kupitia uratibu wa taasisi hiyo.
Amesema kupitia miundombinu iliyowekwa na serikali ya awamu ya sita katika sekta ya afya imekua rafiki kwao kuvutia wageni kuja kupata tiba nchini hali inayosaidia ongezeko la watalii lakini pia ongezeko la fedha za kigeni.
“Sisi kama Vertex tunasaidia kuratibu utaratibu wote wa mgonjwa kuanzia anapotoka kwenye nchi yake mpaka kuahikisha anapata huduma zote za kimatibabu katika hospitali zetu nchini akiwa na usalama wake na mali zake pasipo kupata usumbufu wowote pindi anapofika hospitali”Amesema Swai.
Amesema wameweza kusaidia kuwaunganisha wagonjwa na daktari lakini pia kuwa karibu na mgonjwa huyo mpaka anapomaliza matibabu yake na kurejea nchini kwao lakini kwa mgonjwa ambae anapaswa kufuatiliwa kwa ajili ya kurudi kwa matibabu pia umfuatilia mpaka anakamilisha matibabu yake.
Sambamba na hayo Swai amesema kwa mwaka 2023 wameweza kuwafiki na kuwahudumia wagonjwa 47 kutoka nchi mbalimbali lakini pia ametoa rai kwa wananchi wote nchini kutumia huduma hiyo kwani tiba utalii si kwa ajili ya wageni pekee bali hata wazawa.
“Tiba utalii ni ya wote Watanzania nao wanapaswa kuitumia kwani nchi yetu imejipanga vizuri kuna vifaa vya kisasa lakini pia madaktari wabobezi wapo hivyo ni wasihi watanzania kuja Vertex ili tuwasaidie kuwaunganisha na madaktari bila kupata usumbufu wowote ikiwemo foleni hospitalini”
Kwa upande wake Nasra Samadani Mwanasheri wa Vertex amesema mpaka sasa wanamkataba na hospitali ya Muhimbili na JKCI na wamejipanga kufikia hospitali nyingi zaidi nchini.
Amesema pamoja na mafanikio ambayo wameyapata wanakabiliwa na changamoto kubwa ni kuwafikia wagonjwa wengi zaidi waliopo ndani na kutoa elimu zaidi kutokana na fedha kwani wanajiendesha wenyewe na lengo lao kuhakikisha wanatoa elimu ya tiba utalii katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye barozi za nchi mbalimbali hapa nchini.
Aidha Bi.Samadani ametoa wito kwa wageni na wenyeji kuepuka madalali badala yake watumie taasisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma bora na zenye uhakika kutoka kwa madaktari wabobezi nchini.
Naye,Mmoja wa wagonjwa alitatibiwa na taasisi ya Vertex kutoka Morroco Bwana Mohammed Abdallah amepongeza huduma alizozipata nchini chini ya usimamizi wa taasisi hiyo na kuahidi kuwa barozi mzuri anaporudi nchini kwao.