*************************
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
21.12.2019
AFYA bora ni nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa kipaumbele katika huduma za afya zenye ubora na zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.
Sera ambayo imeendelea kutumika katika kuelekeza utoaji wa huduma za afya ilipitishwa mwaka 1990, ambapo tangu ilipopitishwa, yamekuwepo mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, mabadiliko ya sayansi na technolojia na kuongezeka kwa magonjwa.
Aidha mabadiliko na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Serikali yalitoa changamoto mpya katika utoaji wa huduma za afya na yamechangia kwa pamoja kuifanya sera iliyopitishwa mwaka 1990 kutokidhi mahitaji na matarajio ya sasa na ya miaka ijayo.
Mwaka 1996 marekebisho ya sera yalipitishwa kwa lengo la kuanzisha mfumo mpya wa utoaji na uendeshaji wa huduma za afya katika ngazi ya wilaya, na katika marekebisho hayo ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa afya ulitambuliwa na kupewa msukumo na kukasimu usimamizi wa utekelezaji katika mamlaka za Serikali za Mitaa.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaratibu Mfuko wa Pamoja wa Afya ulioanzishwa mwaka 1996 na kufadhiliwa na wadau 7, ambao ni Denmark, Uswisi (SDC), Ireland, Canada, Benki ya Dunia, UNICEF na Korea Kusini ili kuleta ufanisi na matokea makubwa katika utekelezaji wa miradi ya afya nchini.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2017/2018, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kupitia Sekretarieti ya Uratibu wa Mfukomajadiliano mbalimbali kati ya Serikali na Wadau vimekuwa vikifanywa ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya Serikali jinsi inavyotekeleza kazi zinazogharamiwa na fedha za Wadau.
Anaongeza kuwa wanufaika wa Mfuko huu ni OR -TAMISEMI, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto (Idara kuu ya Afya), Mikoa na Halmashauri zote nchini, ambapo Fedha hizo hugawiwa kwa fomula kwa kuzingatia makubaliano kati ya Serikali na Wadau wanaochangia Mfuko.
‘Serikali kupitia Wizara yake inaendelea na juhudi za kuwaleta pamoja wadau wengine zaidi ili wachangie katika Mfuko huo ili kuleta ufanisi na matokea makubwa katika utekelezaji wa miradi ya afya nchini’’ anasema Waziri Ummy.
Waziri Ummy anasema kuwa Asilimia 90 ya fedha zote hupelekwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, asilimia 6 ya fedha hizo hutumika katika Wizara ya Afya kwa ajili ya masuala ya uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Kisera katika Sekta ya Afya.
Aidha Waziri Ummy anasema kuwa asilimia 3 ya fedha hizo hupelekekwa katika Mikoa kwa ajili ya kugharamia ufuatiliaji katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa na asilimia 1 ya fedha zote hupelekwa Makao Makuu ya OR– TAMISEMI kwa ajili ya kugharamia ufuatiliaji katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy, anasema hadi robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2016/17, kiasi cha Tsh. Bilioni 88.8 kimepokelewa kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya na kati ya fedha hizo, Tsh Bilioni 5.6 zilipokelewa na Wizara ya Afya, Tsh. milioni 865.1 zilipokelewa na OR-TAMISEMI, Tsh. Bilioni 2.6 zilipokelewa na Mikoa na kiasi cha Tsh. Bilioni 79.7 zilipokelewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
‘Fedha hizi hutumika kadiri ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo, ambapo asilimia 33 ya fedha zinazopelekwa katika Halmashauri zinatakiwa kutumika kama nyongeza ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na asilimia 67 ni kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali ambazo zinalenga kuboresha huduma za afya nchini’’ alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy anaongeza kuwa pamoja na kuzingatia vigezo vya usawa katika kugawanya fedha za Mfuko, muelekeo wa Wadau kwa sasa ni kutoa umuhimu kwa ufanisi katika utekelezaji wa kazi zilizokubaliwa ili kuongeza ufanisi katika kazi zinazokubaliwa kuviwezesha vituo vya kutolea huduma za afya kupata fedha kwa wakati na kuweza kufanya maamuzi ya haraka ya kutumia fedha hizo kulingana na mahitaji ya kituo husika.
Akifafanua zaidi Waziri Ummy anasema Wizara imeandaa utaratibu wa kuwezesha fedha za Mfuko kutumwa moja kwa moja kwa vituo vya kutolea huduma za afya ili kuviwezesha vituo kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kulingana na mahitaji yao kwa haraka na Halmashauri zitabaki na jukumu la kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha hizo.
Mfuko wa Pamoja wa Afya ni Mpango mahsusi, ulioanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa fedha kupitia kamati za usimamizi za kutolea huduma za afya katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo ni wajibu wa Mamlaka hizo kuwajengea uwezo watoa huduma za afya utekelezaji wa afua mbalimbali ambazo zinalenga kuboresha huduma za afya nchini.