KAMATI ya Kupitia Kitita cha Mafao cha NHIF cha mwaka 2023 imewatoa hofu wanachama wa NHIF kwamba wataendelea kupata huduma za matibabu kwa sababu mtakaba baina ya mfuko na watoa huduma binafsi haujavunjwa.
Akizungumza Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Baghayo Saqware, amesema walitumia vigezo kushughulikia malalamiko ya watoa huduma binafsi na hakuna aliyeonewa.
“Kamati ilikuwa huru kumsikiliza kila mtu, tulikubaliana kwa pamoja na tuliamua kitita kianze kutumika kwa faida ya nchi na taasisi zetu.
“Kwahiyo Wizara kupitia NHIF iendelee na utekelezaji wa kitita cha mafao kilichoboreshwa cha NHIF cha mwaka 2023 kama ilivyoshauriwa na kamati,” amesema Dk Saqware.
Kamati hiyo imesisitiza kuwa hakuna kituo kitakachositishiwa huduma na kama itatokea ameshauri kitoe taarifa katika mamlaka husika.
Maboresho ya kitita cha mafao cha mwaka 2023 yalianza tangu mwaka 2018 kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya iliyoelekeza mfuko kufanya mapitio ya kitita na bei zake kwa kuzingatia mwongozo wa matibabu Chini toleo la mwaka 2017.