Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF Bernard Konga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Februari 28, 2024.
………………………
Mfuko wa Taifa wa bima ya Afya NHIF umefanya maboresho ya kitita cha mafao kwa wanachama wake huku huduma za kibingwa na bobezi zikipatikana kuanzia ngazi ya kanda.
Akizungumza na waandishi wa habari leo februari 28,2024 jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga amesema kitita cha mafao ni orodha ya huduma za matibabu ambazo zimetolewa kwa wanufaika na bei zake nchini.
Amesema ni miaka 8 sasa tangu maboresho ya mwisho ya kitita cha mafao kinachotumika sasa kufanyika.
“Ni takribani miaka 8 sasa tangu maboresha ya hiki kitita cha mafao kinachotumika kufanyika hivyo kuna umuhimu wa kufanya marejeo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuboresha upatikanaii wa huduma bora kwa wanachama na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo”,amesema Konga.
Amesema wanachama wanaotumia dawa za shinikizo la damu na sukari sasa wanaweza kupata huduma kuanzia ngazi ya chini huku wanachama wanaopata huduma ya uchujaji damu gharama zikiwa zimepunguzwa.
“Huduma za kibigwa na bingwa bobezi kama matibabu ya Moyo,Saratani na Figo sasa zinaweza kutolewa kuanzia ngazi ya kanda na sio lazima mwanachama kwenda ngazi ya Taifa”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa changamoto ya ukosefu wa dawa sasa imeisha kwani dawa mpya zaidi ya 247 zimeongezwa kwenye kitita kipya.
Amesema maeneo yaliyofanyiwa maboresho ili kuleta unafuu ni gharama za usajili na ushauri wa daktari huduma za dawa na tiba za upasuaji na vipimo huku akisisitiza kuwa gharama za maboresho hayo hazimgusi mwanachama bali kati ya NHIF na mtoa huduma.
Maboresho ya kitita hicho yanatarajia kuanza rasmi Marchi Mosi,2024 huku mfuko huo unaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu maboresho zaidi ya kitita hicho.