Tanzania na Urusi zimesisitiza kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa maslahi ya pande zote kupitia ushirikiano wa kidiplomasia ulioanzishwa tangu mwaka 1961. Msisitizo huo umetolewa katika mazungumzo kati ya Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan yaliyofanyika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam Februari 28, 2024. Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika ufuatiliaji wa masuala ya uchumi, biashara, uwekezaji na masuala ya kibinadamu yaliyojadiliwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali Urusi – Afrika uliofanyika nchini Urusi mwaka 2023. Aidha, wamejadili juu ya utaratibu mpya wa kuanzishwa kwa mkutano wa kwanza wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Urusi na Afrika unaotarajiwa kufanyika nchini Urusi mwezi Oktoba mwaka 2024 ambao utaishirikisha Sekretarieti ya Umoja wa Afrika kama sehemu ya marafiki waalikwa wa Urusi. Kadhalika, mkutano huo utaongeza nafasi kwa Nchi za Afrika kujadili utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyokubaliwa na Serikali zao katika nyakati tofauti, sambamba na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za kimkakati. Akiainisha maeneo ya kimkakati, Mhe. Mbarouk ameeleza kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuimarisha sekta ya utalii, hivyo ni wakati sahihi wa kuangalia namna bora ya kuhuisha mifumo mbalimbali inayowezesha kuongeza idadi ya watalii na huduma nyingine za kitalii. Naye Mhe. Avetisyan ameeleza kuwa Urusi imejipanga kuendeleza ushirikiano katika sekta ya utalii kwa kutoa mafunzo kwa kampuni za kitalii na watoa huduma za hoteli ambazo zitaenda sambamba na utangazaji wa filamu ya “Tanzania the Royal Tour”. Pia Mhe. Balozi Andrey Avetisyan ameeleza kuwa Urusi inaunga mkono jitihada za kutangaza utalii ambapo inafanya utaratibu kuliwezesha Shirika la Utangazaji la Urusi la “Russia Today” kuja nchini kuandaa makala za runinga zitakazorushwa nchini Urusi kwa lengo la kuendelea kuhamasisha utalii na utamaduni kwa pande zote mbili. Vilevile viongozi hao wamejadili juu ya umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya elimu pamoja na kuendelea kutoa hamasa kufuatia fursa za ufadhili za masomo ya muda mrefu na mfupi zinazotolewa na Serikali ya Urusi kwa Watanzania |
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akizungumza na Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan alipomtembelea katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 28 Februari, 2024. |
Maafisa kutoka Ubalozi wa Urusi walioambatana na Mhe. Avetisyan wakifatilia mazungumzo. |
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo. |
Mazungumzo yakiendelea |
Balozi Mbarouk akiagana na Mhe. Avetisyan. |