Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema barabara zote ambazo zipo chini ya mitandao ya mkoani hadi sasa zipo kwa ajili ya wakandarasi wazawa pekee yao kwa maana ya fedha zipo mikoani na ni soko lisilopungua bilioni 550 hapo hazijawekwa za TARURA kwa mwaka ambazo ni takribani bilioni 229.
Amesema fedha kwa ajili ya wakandarasi wazawa kwa upande wa malipo ya madeni serikali inaendelea na kazi ya kuchakata ili malipo yasichukue muda mrefu yawe yamelipwa kwa wakandarasi.
Bashungwa ameyasema hayo leo Februari 26, 2024 wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya Mpango wa Mafunzo kwa Wahandisi Wahitimu (SEAP) wenye lengo la kuwajengea umahili wahandisi wanaomaliza vyuo vikuu, huku wahandisi zaidi ya 300 waliofuzu mafunzo hayo wakika kiapo umahili pamoja na uzinduzi wa mpango wa awamu ya tatu wa ufadhili huo kwa wahandisi wa kike katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua juhudi za wahandisi kuleta maendeleo katika Taifa na wanafanyia kazi changamoto zinazokabili mradi wa SEAP.
Amesema tukio hilo ni muhimu na mradi wa SEAP utasaidia kutatua changamoto ambazo wametaja na kuwawekea misingi mizuri wahandisi.
Pia ameiagiza Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuhakikisha wanawachukulia hatua kali wakandarasi wanaohatarisha maisha ya watanzania kwa kujenga barabara zisizozingatia viwango na ambao leseni zao za uhandisi zimeisha kabla ya Marchi 31, 2024.
Ametoa wito kwa wahandisi wote nchi kuzingatia miiko ya taaluma yao kwa sababu wahandisi ni watu muhimu nchini.
Pia amewataka wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini kuzingatia taaluma yao na kuitumia vizuri ili kusaidia sekta hiyo ya ujenzi na nchi kukua kiuchumi.
Amesema amezungumza na Benki ya Dunia miradi mikubwa ambayo inafadhiliwa na benki hiyo, katika kilometa 500 za barabara ambazo wamepata ufadhili wao, robo kilomita hizo watenge kwaajili ya wakandarasi wa ndani vigezo viendane na hao wakandarasi.
Kwa upande wake msajili wa Bodi ya Wanandisi, Mhandisi Benard Kavishe amesema pamoja na sekta hiyo kuendelea kukua kwa Kasi upande wa wasichana idadi bado hairidhishi huku baadhi ya wadau kutoka Tarura, Tanroad, sekta binafsi na ILO nao wakiahidi kuendelea kuunga mkono mpango huo wa kuwajengea umahili wahandisi.
Amesema Bodi hiyo pia ipo mbioni kuanzisha shule ya taaluma hiyo ili kuwafikia vijana wanaohitimu wengi zaidi.