Muonekano wa Treni ya Umeme ya Kisasa (SGR).
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 26/2/2024 Jijini Dar es Salaam wakati akiwa katika majaribio ya Treni ya umeme ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa ajili ya kuangalia miundombinu, mifumo pamoja vifaa vitakavyotumika kabla ya kuanza kufanya rasmi mwezi Julai, 2024.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bi. Jamila Mbarouk akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 26/2/2023 kuhusu majaribio ya treni ya umeme y Kisasa ambayo inatarajia kuanza kutumia mwezi Julia, 2024.
Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi akiwa ndani ya Treni ya umeme ya Kisasa (SGR) wakati ikiwa katika majaribio kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa ajili ya kuangalia miundombinu ya reli, mifumo, vifaa vitakavyotumika kabla ya kuanza kutumika rasmi.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa (kushoto) akiwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi wakati wakienda kupanda Treni ya umeme ya Kisasa (SGR) kwa ajili ya kufanyiwa majaribio.
Baadhi waandishi wa habari pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wakiwa ndani Treni ya umeme ya Kisasa (SGR) wakati wakifanya majaribio wakitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.
Muonekano wa ndani ya Treni ya umeme ya Kisasa (SGR).
Muonekano miundombinu ya Treni ya Umeme ya Kisasa (SGR).
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Reli Tanzania (TRC) imefanya majaribio ya Treni ya umeme ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa ajili ya kuangalia miundombinu ya reli, mifumo, vifaa vitakavyotumika kabla ya kuanza kufanya rasmi mwezi Julai, 2024.
Katika majaribio ya usafiri wa SGR viongozi mbalimbali wameshiriki akiwemo Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi, Wafanyakazi wa TRC, wanahabari kutoka vyombo mbalimbali, jambo ambalo limeonekana linakwenda kuleta tija katika kuchochea shughuli za uchumi baada ya kuanza kufanya kazi
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 26, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa, amesema kuwa mradi huo unatarajia kuanza kufanya kazi mwezi Julia, 2024, huku akieleza miundombinu ya mradi wa SGR umekamilika kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro.
Bw. Kadogosa amesema amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.
“Leo ni muendelezo wa majaribio ya treni ya umeme ya kisasa (SGR) tunawaambia watanzania reli yao inaelekea kuanza kutumika rasmi kama Mhe. Rais Dkt. Samia alivyoyatoa ya maagizo kuwa mwishoni mwa mwezi wa saba tuwe tumeshaanza kutoa huduma ya usafiri huu kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma” amesema Bw. Kadogosa.
“Tunajenga kwa vipande kuna kipande cha kwanza cha kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, kipande kingine cha pili cha kutoka Morogoro mpaka Makutupora, vipande vingine ujenzi unaendelea kutoka Makutupora kwenda Tabora,Isaka, Mwanza na Tabora kwenda Kigoma” amesema Bw. Kadogosa.
Amefafanua kuwa hivi karibuni wamesaini mkataba wa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa SGR
kutoka Uvinza kwenda Msongati kwa maana ya kuunganisha na Burundi baadaye itaenda mpaka DRC Congo,”amesema Bw. Kadogosa.
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi, amewatoa hofu watanzania kuhusu huduma ya umeme katika utekelezaji SGR, huku akieleza kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeingia makubaliano na TRC ili kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika.
Bw. Matinyi amesema kuwa TANESCO wametoa upendeleo katika kufanikisha huduma ya usafiri SGR ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa huduma ya usafiri huo.
“TANESCO imeunganishwa umeme kutoka grid ya Taifa ambao hautakuwa na usumbufu, serikali ilivyaamua kuleta treni ya umeme ya kisasa ilikuwa na uhakika kutakuwa umeme wa kutosha” amesema Bw. Matinyi.