Na Sophia Kingimali
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa ametoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa zitakazozalishwa na mradi wa ujenzi matenki 15 na miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za mafuta huku akitaka wawe waadilifu na kuweke uzalendo mbele.
Aidha amewataka TPA na wizara ya Uchukuzi kusimamia kwa makini miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuendana na thamani halisi ya fedha ya mradi husika.
Hayo ameyasema leo Februari 26,2024 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa usanifu na ujenzi wa matenki na miundombinu ya kupokea,kuhifadhi na kusambaza bidhaa za mafuta ya petroli katika bandari ya Dar es salaam.
Amesema utiaji saini wa mkataba huo ni jambo la kihistoria kwa nchi kwani ni zaidi ya miaka 10 wamekuwa wakiangika na mradi huo.
ameainisha muda wa utekelezaji wa mradi huu ni miaka miwili ambapo katika kipindi hiko mkandarasi atajenga matenki kumi na tano (15) yenye mita za ujazo wa 420,000 m3 pamoja na miundombinu yake.
Aidha amesema kuwa mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 678.6 ambazo atapewa Mkandarasi M/S China Railway Major Bridge Engineering Group Co. Ltd. na M/S WUHUAN Engineering Co. Ltd, ya china ilipendekezwa kupewa zabuni.
Sambamba na hayo Prof.Mbarawa amesema TPA inasimamia miradi ya shilingi Tilion1.4 kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu mamlaka ya Bandari nchini (TPA)Plasduce Mbossa amesema ujenzi wa tanki hizo utasaidia Kupungua kwa gharama zinazotokana na meli kukaa bandarini muda mrefu (demurrage charges) kwani kwa sasa meli za SPM zinatumia wastani wa siku 11 mpaka 12 kushusha mafuta ambapo kwa sasa kushusha unatumia dola za kimarekani 25,000 kwa siku.
Amesema Ujenzi wa matenki unategemewa kurahisisha ushushaji wa mafuta na kupunguza hadi siku 3 mpaka 4. Hii itafanana na hali ya sasa ya TAZAMA ambapo wanatumia masaa 48 kushusha mafuta melini kupitia SPM. Kwa maana nyingine, kutakuwa na saving ya wastani wa siku 8 ambazo ni sawa na dola za kimarekani 200,000 (US$ 25,000 x 8). Kwa kuwa gharama hii kwa sasa inakwenda kwenye bei ya pump, hali hii pia inategemewa kupunguza bei ya mafuta kwa mwananchi wa kawaida.
Ameongeza kuwa matanki hayo yatasaidia Kuondoa tatizo la upotevu wa mafuta (Outturn Losses) katika Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza malalamiko miongoni mwa wafanyabiashara wa mafuta.
“Ujenzi wa haya matanki 15 utasaidia Kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato. Kwa kuwa mafuta yote yatapokelewa na kupimwa vizuri yakiwa sehemu moja (tank farms) na kuwa chini ya Mamlaka ya Bandari kabla ya kuyasambaza, hali hii itaimarisha udhibiti wa mapato ya Serikali kwa kuzuia mianya ya ukwepaji kodi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na bidhaa za mafuta zinazoingia nchini”,Amesema.
Ameongeza kuwa Kuimarisha hifadhi ya mafuta nchini. Matenki ya mafuta yatakayojengwa na TPA yataihakikishia Serikali hifadhi ya mafuta ya kutosha. Hii itaondoa changamoto ya sasa ambapo uwezo wa kuhifadhi mafuta nchini ni wa siku 15 tu na uwezo huu ni wa matenki ya Makampuni binafsi ya mafuta. Hali hii pia itaongeza uaminifu miongoni mwa wafanyabiashara wanaotaka kusafirisha mafuta nje kwa kuwa wanaweza kuhifadhi mafuta yao katika matenki ya Bandari.
Amesema Ujenzi wa matenki hayo ya mafuta pia yatahakikisha usalama wa uwepo wa mafuta (security of supply) na pia itasaidia uanzishwaji wa Strategic Petroleum Reserve (SPR). Kwa kuwa mafuta ni moja ya bidhaa ambayo inachangia kiasi kikubwa cha exchange rate, uwepo wa SPR utaleta uimara wa sarafu ya Tanzania dhidi ya dola za kimarekani.
“Uwepo wa uhakika wa mafuta nchini kutokana na ujenzi wa tank farms and gati la kupokea na kupakua mafuta pia inaweza kupunguza mfumuko wa bei (inflation) na kuleta nafuu kwa mwananchi wa kawaida. Hii inatokana na ukweli kwamba kupanda kwa bei ya mafuta kunasababisha kwa kiasi kikubwa kupanda kwa bidhaa nyingine,”Amesema Mbossa.
Aidha amesema kuwa Mradi utachochea mashirika yanayoshughulika na mafuta kuanzisha Kituo cha usambazaji Mafuta (Hub) kwenda nchi za jirani kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo na hivyo kuifanya Tanzania kua kituo cha soko la biashara ya mafuta.
Naye,mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu ametoa rai kwa wizara ya uchukuzi na TPA kuhakikisha mradi huo pindi utakapoanza uhakikishe unatoa kipaumbele kwa wananchi wazawa ili waweze kupata ajira.