Kamishna Mkuu wa hifadhi ya Ngorongoro Richard Rwanyakato Kiza akizungumza katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Jukwaa la Wahariri na NCAA kilichofanyika Mafao House Ilala jijini Dar es Salaam Februari 26, 2024.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Thobias Makoba akizungumza katika kikao kazi hicho.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri akifafanua baadhi ya mambo katika kikao hicho.
Waandishi nguli wa habari nchini Tanzania ambao kwa sasa ni wastaafu kulia ni Salva Rweyemamu na kushoto ni Said Nguba wakishiriki katika kikao hicho kama wageni waalikwa.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Thobias Makoba akiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro NCAA Bw. Khamis Dambaya wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa ya Kikaokazi hicho.
………………………
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro NCAA inajivunia mafanikio makubwa waliyoyapata ambayo yamechagizwa kwa kiasi kikubwa na filamu ya The Royal Tour iliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza jijini Dar es salaam Februari 26,2024 katika kikao kilichoandaliwa na ofisi ya Msajili wa hazina na Jukwaa la Wahariri Kamishna Mkuu wa hifadhi ya Ngorongoro Richard Rwanyakato Kiza amesema mapato kutokana na utalii yameongezeka kutoka bilioni 31 mwaka 2021 mpaka kufikia bilioni 171 kwa mwaka 2022/2023.
Amesema kupitia filamu ya The Royal Tour imepelekea ongezeko kubwa la watalii kutoka watalii 191,914 mwaka 2021 na kufikia watalii 752,332 mwaka 2022/2023 ambapo idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia watalii milioni moja kwa mwaka 2023/2024.
“Tunatarajia kuwa na idadi kubwa ya watalii katika hifadhi ya Ngorongoro kwani mpaka sasa idadi imeongezeka kwa asilimia 10 ikilinganishwa na idadi ya wageni kwa mwaka 2023/2024 ambapo na mapato yanategemea kuongezeka zaidi na kufikia bilioni 200 kwa mwaka “,amasema.
Amesema ongezeko la mapato linatarajiwa mpaka kufikia bilioni 200 kwani kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2023/2024 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni123 tayari zimekusanywa.
Amesema kuongezeka kwa mapato hayo kumesababishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Rais katika kuinua sekta ya utalii lakini pia kupitia filamu ya Royal Tour.
Ameongeza kuwa serikali imetenga kiasi cha fedha bilioni 69 kwa ajili ya ujenzi wa tabaka gumu la kipande cha barabara yenye urefu wa Km. 29 kutoka lango kuu la kuingia hifadhi ya Ngorongoro.
“Katika kuimarisha miundombinu pamoja ongezeko la watalii tunamshukuru Rais wetu kwani alitoa fedha ya uviko bilioni 6.6 ambayo ilitumika kujenga miundombinu ya barabara na kununua vifaa vya ujenzi,”amesema.
Akizungumzia zoezi la kuhama kwa hiyari kwa wananchi kutoka hifadhi ya Ngorongoro amesema mpaka kufikia Februari 25,2024,jumla ya kaya 1042 zenye watu 6461 na mifugo 29,919 wamehama kwa hiyari.
Amesema hadi kufikia januari 2023 wakati zoezi la awamu ya kwanza linakamilika kaya zipatazo 551 zenye watu 3010 na mifugo 15,521 walikua wamehama kutoka Ngorongoro na kwenda kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni.
“Awamu ya pili ya zoezi ilianza mwezi Julai, 2023 kwa mpango wa kujenga nyumba 5000 ambazo zinajegwa katika kijiji cha Msomera,nyumba 1000 zinajengwa katika kijiji cha Sayuni wilaya ya Kilindi na nyumba 1500 zinajengwa katika kijiji cha Kitoi B kilichopo wilaya ya Simanjiro.
Picha zikionesha wahariri mbalimbali wakishiriki katika Kikaokazi hicho.