Na. Zillipa Joseph, KATAVI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Kassim Majaliwa amezindua kituo cha Redio ya kijamii Mpimbwe Fm ikiwa ni moja ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM) katika Jimbo la Kavuu Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Majaliwa amesema kuwa kuzinduliwa kwa kituo hicho cha Redio kutakuwa chachu ya kuleta Maendeleo katika Halmashauri hiyo ya Mpimbwe pamoja na kutangaza mafanikio yanayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri ya Mpimbwe kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM).
“kituo hiki kitumike kutangaza mipango inayotarajiwa kutekelezwa katika Jamiii kutoka kila Idara sambamba na kupunguza changamoto za wananchi watakazokuwa nazo kwa kuuliza maswali katika vipindi vya redio na kujibiwa na Wataalam wa kila idara”alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa
Amempongeza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard kwa kuwezesha kufunguliwa kwa kituo cha Redio Mpimbwe huku akikumbusha ombi la Mbunge wa Jimbo la Kavuu Geofrey Pinda kufunguliwa kituo cha televisheni ili kuendelea kuimarisha mawasiliano na upatikanaji wa Habari katika Halmashauri hiyo ya Mpimbwe.
Nae mbunge wa Jimbo la kavuu Geofrey Pinda amewaasa wakazi wa Halmashauri ya Mpimbwe kuitumia na kuisikiliza redio Mpimbwe kwa kupata habari,elimu na mafunzo kutoka kwa wataalam mbalimbali katika Halmashauri hiyo.
Amesema kituo hicho cha redio Mpimbwe kimejengwa na serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote serikalini (UCSAF) kwa gharama ya shilingi milioni 230.