Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP. THEOPISTA MALLYA akikabidhi sare za shule kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya Msingi Katete iliyopo kata ya Mpemba Mjini Tunduma Mkoani Songwe. Tarehe 23 Februari 2024
Kamanda Mallya amekabidhi sare hizo alipotembelea shule hiyo na kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili wawe wataalamu wa fani mbalimbali watakaotegemewa katika shughuli za maendeleo ya Taifa letu.
……
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Katete iliyopo Mpemba Mjini Tunduma mkoani Songwe wametakiwa kujiepusha na vishawishi vya mafataki wanaotaka kukatisha ndoto ya safari ya masomo yao.
Hayo yalisemwa Februari 23, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Theopista Mallya alipokuwa akitoa elimu juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa Shule hiyo.
“Najua mpo karibu na barabara ya Mbeya -Tunduma na kuna muingiliano mkubwa wa watu hivyo niwatake kujiepusha na tabia ya kuomba lift kwa watu msiowajua wala kupokea zawadi toka kwa watu msiowafahamu ili kuepuka kufanyiwa vitendo vya ukatili” alisema Kamanda Mallya.
Aidha, Kamanda Mallya aliwataka wanafunzi wa Shule hiyo kuwa makini katika matumizi ya barabara hasa uvukaji salama wa barabara kwani eneo hilo lina historia ya mmoja wa mwanafunzi wa Shule hiyo kupoteza maisha kwa kugongwa na Gari akiwa anavuka barabara.
Aliwataka walimu na wananchi wa mkoani Songwe kuungana na Jeshi la Polisi kupinga ukatili ili ujumbe ufike kwa wepesi kwa jamii jambo ambalo litapelekea kupunguza ukatili katika mkoa huo.
Kamanda Mallya aligawa sare za Shule kwa watoto wenye mahitaji maalumu na kuwaambia Polisi ni rafiki pia ni rafiki wa watoto kwa hiyo wasiogope kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa Jeshi la Polisi pindi waonapo viashiria au wafanyiwapo vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.