Mkuu wa wilaya ya Mbulu Ndugu Kheri James mapema leo amekabidhi pikipiki nane kwa Jumuiya za watumiaji maji ngazi ya jamii-CBWSOs, ikiwa ni mkakati wa RUWASA wilayani Mbulu kuimarisha utendaji wa jumuiya hizo muhimu.
Akitoa taarifa ya zoezi hilo Meneja wa RUWASA wilaya ya Mbulu Muhandisi Onesmo Mwakasege, ameeleza kuwa lengo la kukabidhi pikipiki hizo ni kurahisisha ukusanyaji na ufatiliaji wa mapato, Kufika kwa wakati kwa ajili ya matengenezo na marekebisho ya miundombinu, kupunguza gharama za usafiri kwa mafundi na kuwafikia Wananchi kwa haraka na kwa wakati.
Katika hotuba yake kwa watumishi na viongozi wa jumuiya za watumia maji katika zoezi hilo, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ameipongeza RUWASA kwa kazi kubwa na nzuri ya ujenzi wa miradi ya maji na usimamizi pamoja na uendeshaji wa miradi ya maji wilayani Mbulu.
Aidha Kheri James ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na kuzijengea uwezo taasisi ili kufanya kazi kwa ufanisi itaendelea ili kuhakikisha sekta zote muhimu zinakuwa na nyenzo bora na muhimu za kuchochea huduma kwa Wananchi.
Pamoja na mambo mengine, Kheri James amewasihi watumishi na viongozi wa CBWSOs kuzitunza vyema pikipiki hizo, Kuzitumia kwa kazi ilio kusudiwa na kuzingatia sheria kwa Usalama wa chombo na mtumiaji.
Jumuiya za watumia maji ngazi ya jamii-CBWSOs zilizokabidhiwa pikipiki kwa siku ya leo ni; EYAESH, MASIEDA, HAYDERER, DINAMU, YAEDA, GIDHIM, MARETADU na GEMA. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha jumuiya zote zinapewa pikipiki hizo katika awamu ijayo.
Shughuli ya makabidhiano ya pikipiki hizo, imehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa wilaya ya Mbulu, Kamati ya Usalama, viongozi wa jumuiya za watumia maji, watumishi pamoja na Wananchi.