NA BALTAZAR MASHAKA MWANZA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),mkoani Mwanza,katika kuongeza idadi ya wanachama kimewahimiza watu kuchukua kadi mpya za kielektroniki na kusajiliwa katika mfumo huo kwa kuchangia gharama ya sh.2,000.
Rai hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na Katibu wa Itikadi,Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa Mwanza,Prudence Sempa,leo wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za kata za Buzilasoga wilayani Sengerema na Mhande katika Wilaya ya Kwimba.
Amesema baada ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata za Buzilasoga na Mhande kumalizika,wana CCM wahakikishe wanawahimizwa kuchukua kadi za kielektroniki kwa sh.2,000 na kusajiliwa katika mfumo huo wa kisasa.
“Ingawa bei halisi ni sh,5000 watu wajitokee kuchukua kadi za kisasa kwa kuchangia sh. 2,000 ili kila mwana Chama awe na kadi hiyo iliyounganishwa na mifumo ya huduma mbalimbali, lengo ni kuongeza idadi ya wanachama ambao ni mtaji wa kisiasa,”amesema Sempa.
Amesema baada ya uchaguzi mdogo wa udiwani kumalizika, watu wahamasishwe wakajiandikishe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,wapate fursa ya kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu lakini pia wasio na vyama na wanachama wa vyama vingine vya siasa wajiunge na CCM.
Sempa amesema kadi hizo za kisasa za CCM zina faida nyingi kulinganisha na za vyama vingine, kutokana na kuunganishwa na mifumo ya huduma za matibabu,NIDA, fedha,haki za usafiri na huduma zingine.
Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi huyo tayari Mkoa wa Mwanza umepokea kadi za kielektroniki 79,986 na kuwataka makatibu wa wilaya kuchangamkia fursa hiyo huku akiwaasa wahakikishe fedha za mauzo ya kadi hizo zinawasilishwa makao makuu zichapwe zingine.
Amewataka wananchi na wana CCM kuchapa kazi ili kuwaunga mkono viongozi wa Serikali na Chama na kuwatia moyo wa kuendelea kuwahudumia na kuwatumikia kwa ajili ya maendeleo ikizingatiwa kazi ni kipimo cha utu.