Mkuu wa Kitengo cha Sera na Usimamizi wa Maliasili wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza akitoa ufafanuzi juu ya masuala ya uhalifu dhidi ya wanyamapori.
Kakakuona
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo akifafanua jambo wakati wa semina.
Washiriki wa mafunzo ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wakiwa katika picha ya pamoja.
…………………..
NA SIDI MGUMIA, BAGAMOYO
Mashirika mbalimbali ya kimataifa yamekuwa na mkakati madhubuti wa kulinda rasilimali hasa wanyama akiwamo kakakuona ambaye kwa sasa yupo hatarini kutoweka.
Hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na usafirishaji haramu wa wanyamapori kutokana nchi za Afrika ambazo nyingi zikitajwa kama sehemu ya uchochoro wa ukusanyaji wa wanyama hao na kuwasafirisha kwenda nchi za Asia na kwingineko.
Kutokana na hali hiyo, Shirika la Misaada la Marekani USAID kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wameendelea kuwa sehemu ya kumlinda mnyama huyo na wanyama wengine walio kwenye tishio la kutoweka duniani.
Mkuu wa Kitengo cha Sera na Usimamizi wa Maliasili wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza anaweka wazi kuwa ipo haja ya jamii kushiriki kwa pamoja katika kuwalinda wanyama walio kwenye hatari ya kutoweka akiwemo Kakakuona na Tembo.
“Hawa wanyama wana umuhimu mkubwa sana katika maisha ya binadamu na viumbe wengine, kutoweka kwao kutatulazimisha kuja kutumia picha ili kuwaonesha watoto wetu aina za wanyama hawa, hawatakuwepo,” amesema.
Kaka kuona ni miongoni mwa waathirika wakuu wa biashara haramu, anawindwa zaidi katika nchi nyingi duniani na Tanzania ikiwemo.
Kakakuona anapatikana zaidi katika nchi za Afrika na Kusini Mashariki mwa Asia. Aina mbili kati ya nane ya mnyama huyo wameorodheshwa kuwa hatarini, wakiwekwa katika orodha nyekundu ya aina ya wanyama walio hatarini.
Ukweli ni kwamba mnyama huyo anashika nafasi ya kwanza katika orodha ya mamalia wanaosafirishwa kwa magendo duniani.
Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Uhifadhi wa Mazingira ilibaini kuwa kati ya mwaka 2000 hadi 2019, karibu Kakakuona 900,000 walisafirishwa katika nchi mbalimbali duniani, huku China ikitajwa kuwa mnunuzi mkuu.
Mwaka 2009 mji wa Borneo nchini Malaysia zilikamatwa tani 27 za nyama ya Kakakuona iliyokadiriwa kuwa na thamani ya paundi milioni 1.6.
Kakakuona ndiye mamalia pekee mwenye magamba duniani, chakula chao kikuu ni mchwa na wadudu ambao hufanikiwa kuwakamata kutokana na ulimi wao mrefu.
Pamoja na hilo Kakakuona ni wanyama wadogo na mwenye mwili mkubwa hukadiriwa kuwa na urefu wa mita 1.8 na uzito wa kilo 30.
Mnyama huyu anaponzwa na magamba na nyama yake. Magamba yake hutumiwa zaidi kwenye dawa za jadi za Kichina, watumiaji wanaamini magamba na kucha zake husaidia kutibu magonjwa ya pumu na saratani na nyama yake inadaiwa kuongeza nguvu mwilini, ingawa hadi sasa hakuna tafiti za kitaalamu zilizothibitisha hayo.
Akitoa uelewa kwa waandishi wa habari za mazingira juu ya namna ya kupambana na uhalifu dhidi ya wanyamapori, Mgaza amekiri kuwa Kakakuona wamekuwa wakiwindwa sana hali inayotishia kutoweka kwao.
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umelenga kulinda shoroba saba nchini zinazotumiwa na wanyama katika kusaka malisho na maji, lakini pia utatumika katika kutoa elimu ya kukabiliana na uhalifu dhidi ya wanyamapori.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa JET, John Chikomo ameongeza kuwa katika mapambano dhidi ya uhifadhi wa maliasili, wanyama na mazingira kwa ujmla, elimu ya mazingira na haswa uhifadhi bado inahitaji iepelekwe kwenye jamii lakini pia kusisitiza uwepo wa ushirikishwaji wa sekta na wizara mbalimbali katika masuala ya mazingira.
Nae Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru alisisitiza kuwa ni jukumu la waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kuchechemua na kuziibua changamoto za shoroba na kuelimisha jamii juu ya athari zake lengo likiwa ni kupeleka mambo mapya kwa watunga sera ili wayafanyie kazi mapendekezo yakutatua changamoto za mausala ya uhifadhi kwa ujumla wake.
JET imefanya mafunzo ya siku mbili na waandishi wa habari 20 mjini Bagamoyo, mkoani Pwani kwa ajili ya kuwaongezea uwezo na kuwahamasisha kuandika masuala yanayohusiana na masuala ya uhifadhi wa bioanuai.
Mafunzo hayo ambayo yalianza Januari 15, 2024 yaliratibiwa na JET chini ya ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili.