NA VICTOR MASANGU KIBAHA
Viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) wametakiwa kuachana kabisa na tabia ya kulalamika kwa kutumia mitandao ya kijamii na badala yake wanatakiwa kuzingatia vikao halali vya kikanuni au kumtafuta muhusika ili kupata ufumbuzi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini Issack Kalleiya wakati wa kikao kazi kilichofanyika Katika Ukumbi wa CCM Wilaya na kuwakutanisha madiwani wa kata zote 14 za Kibaha Mjini na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
Katibu huyo alisema kuwa viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa kufuata maelekezo ya chama kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na sio vinginevyo kulalamika kwenye mitandao ya kijamii.
Katibu huyo alisema kwamba viongozi CCM wanatakiwa wajiweke tayari kwa uchaguzi na kuacha kulalamika kwa watu ambapo jambo hilo limekua linashika kasi kwa baadhi ya viongozi kutoa siri za vikao na kuwapa watu ambao hawahusiki.
Katibu wa CCM amesisitiza kuwa kwa sasa Wilaya ya Kibaha Mjini ina jambo kubwa la Uchaguzi ww Udiwani Kata ua Msangani hivyo amewataka wote kujiweka tayari kwa kushiriki katika Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi 20,2024.
Aidha, Katibu Kalleiya amewataka Madiwani pamoja na wenyeviti wa Serikali za Mitaa kushiriki katika Uchaguzi wa Udiwani Kata ya Msangani pindi watakapohitajika ikiwemo kusaidia kunadi Chama wakati wa kampeni na kutafuta kura kwa wananchi ili CCM ishinde kwa kishindo.
Katibu Wa CCM amesema, wote wanatakiwa wawe tayari ambapo ratiba ya uchukuaji na urudishani wa fomu za Uchaguzi unaanza tarehe 21/02/2024 hadi 23/01/2024.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha na Diwani wa Kata ya Sofu Mhe. Mussa Ndomba amepokea maelekzo hayo kwa kuahidi kushirikiana na Chama katika Uchaguzi huu mdogo wa marudio ili kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo.
Pia, amesema maelekezo yote yaliyotolewa watayafanyia kazi na kwa sasa watakuwa wanakaa vikao pamoja katika ya madiwani na wenyeviti wa Serikali za Mitaa sambamba na Mkurugenzi ili kujadili masuala mbalimbali na kuweza kutatua changamoto zilizopo katika mitaa yao.
Kikao hicho kilitoka na kauli moja ya CCM Moja KIbaha Moja ambapo wote Madiwani na Wenyeviti walikubali kushirikiana katika kukijenga Chama, kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.