WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 20,2024 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Desemba 2023.
Na.Alex Sonna-DODOMA
IMEELEZA kuwa kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa hizo imechangia kuwepo kwa ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa leo Februari 20,2024 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama,wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mamlaka ya kupambana dhidi ya dawa za kulevya kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Desemba 2023.
Mhe.Mhagama amesema kuwa hivi sasa kumekuwepo na ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini.
“Sababu ya ongezeko hilo ni kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya .Takwimu kutoka kwenye vituo vya MAT zinaonesha jumla ya waraibu wapya 2,219 wamejiunga na tiba kwa mwaka 2023 na kufanya idadi ya waraibu wanaopata tiba ya Methadone kufikia 15,915,”amesema Waziri Mhagama
Aidha Waziri Mhagama amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata kilogramu 1,965,340.52 za aina mbalimbali za dawa za kulevya nchini ambapo watuhumiwa 10,522 wamekamatwa katika kipindi hicho huku wanaume wakiongoza kujihusisha na biashara hiyo haramu.
“Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 kilogramu 1,965,340.52 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo. Aidha, jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa”amesema Mhagama
Amesema kuwa kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11.
Hata hivyo amesema kuwa serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Waziri Mhagama amesema kuwa elimu imeendelea kutolewa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya viongozi wa dini, viongozi wa kimila, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, maafisa forodha na wakulima hasa katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha bangi na mirungi.
”Elimu ya dawa za kulevya imeendelea kutolewa kupita vyombo vya habari, makongamano na maonesho ya kitaifa na kimataifa.”amesema
Amesema kuwa mwaka 2023 kituo kimoja kimefunguliwa mkoani Morogoro katika gereza la kihonda ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2023, jumla ya vituo 16 vilikuwa vinatoa huduma kwa walengwa.
Amesema vituo vingine viwili katika wilaya ya Muheza – Tanga na Chalinze – Pwani vinatarajia kukamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka huu. Vituo vingine vitatu vitaanza kujengwa katika mikoa ya Shinyanga, Kilimanjaro na Pwani (Mkuranga).
‘Serikali iko kwenye hatua za mwisho za ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za Tiba na utengamao (Rehabilitation centre) katika jiji la Dodoma ambacho mbali na huduma za matibabu pia yatatolewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha waraibu kujitegemea kimaisha baada ya kukamilisha safari ya matibabu yao.’amesema