Na Mwandishi wetu, Tunduru
HOSPITALI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma,imeanza kampeni maalum ya upimaji wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wanafunzi wa shule zote za msingi na sekondari wilayani humo.
Kampeni hiyo imeanza kwa wanafunzi wanaoishi bweni,ambapo watakaokutwa na maambukizi ya TB wataanzishia dawa kama mkakati wa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika wilaya ya Tunduru.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole wakati wa kampeni ya uelimishaji,uibuaji na uchunguzi wa ugonjwa huo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Kiuma.
Dkt Kihongole alisema,wanaamini kuwa wanapotoa elimu ya kifua kikuu kwa watoto hasa wanafunzi ni rahisi sana ujumbe kuwafikia watu wengi katika jamii ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na ugonjwa wa Tb.
Alisema,watoto wanapokuwa likizo wanakuwa kwenye muingiliano na wanakutana na watu mbalimbali na miongoni mwao wapo wanaougua kifua kikuu,hivyo wao kuwa katika hatari ya kupata maambukizi bila kujitambua,na wanaporudi shuleni ni rahisi kuambukiza wengine.
“Ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa kushirikiana na idara ya elimu ya msingi na sekondari kwa pamoja tumeamua kwenda shule hadi shule na tumeanza na wanafunzi wanaoishi bweni kwa ajili ya kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa vimelea vya Tb”alisema.
Alieleza kuwa,katika kampeni hiyo wanafunzi watakaobainika kuwa na maambukizi ya kifua kikuu watapata matibabu mapema ili wasiambukize wengine na kama hakuna walioambukizwa ni faraja kwa idara ya afya na wilaya ya Tunduru.
Alisema,kupitia kampeni mashuleni wanaamini wamepata mabalozi wazuri watakaokwenda kutoa elimu ya kifua kikuu kwa jamii na kutekeleza kwa vitendo mkakati wa serikali wa kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Mwalimu wa shule ya sekondari Kiuma Hosea Shukurani,ameipongeza Hospitali ya wilaya Tunduru kitengo cha kifua kikuu na ukoma kupeleka elimu ya Tb kwa shule hiyo kwani itawasaidia wanafunzi na walimu kuwa na uelewa kuhusu dalili na namna ya kujikinga.
“sisi kama walimu tumefurahi sana elimu hii kutufikia bure bila gharama yoyote,tutaitumia kuhakikisha katika shule yetu hakuna mwanafunzi atakayeambukizwa ugonjwa huo”alisema Shukurani.
Mwanafunzi wa shule hiyo Tulibia Raynald alisema,elimu waliyoipata itakuwa mwanzo wa kufanya vizuri katika masomo yao kwa kuaminikwamba hakuna mwanafunzi atakayekatisha masomo kutokana na kuugua ugonjwa huo.
Alisema,hatua hiyo itawawezesha kupeleka elimu ya Tb kwa familia na jamii kwa ujumla na watakuwa mabalozi wazuri wa serikali katika mapambano ya ugonjwa huo unaotajwa kupoteza maisha ya watu wengi hapa nchini.