WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yatakayofanyika jijini Mwanza Mwaka huu,kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt.Leonard Maboko.
Sehemu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama,wakati akitoa taarifa kuhusu maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yatakayofanyika jijini Mwanza Mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt.Leonard Maboko,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yatakayofanyika jijini Mwanza Mwaka huu.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yatakayofanyika jijini Mwanza Mwaka huu,kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt.Leonard Maboko.
PICHA NA ALEX SONNA-FULLSHANGWEBLOG
…………………………
Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inaratibu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo hufanyika Tarehe Mosi Desemba kila mwaka tangu ilipoasisiwa kwa uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia kudhibiti UKIMWI Duniani (UNAIDS).
Malengo ya Maadhimisho haya ni pamoja na:
- Kutoa fursa ya kutathmini hali halisi na mwelekeo wa kudhibiti Virusi Vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI kitaifa na kimataifa
- Kutafakari changamoto, mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya kudhibiti VVU na UKIMWI.
- Kutafakari na kutekeleza Kauli mbiu inayotolewa kila mwaka kulingana na vipaumbele vya kidunia na kikanda na kitaifa kwa muktadha wa kitaifa.
- Kuwakumbuka watu wote waliopoteza maisha yao kutokana na UKIMWI pamoja na kuwajali yatima waliotokana na vifo vinavyohusiana na UKIMWI.
- Kuwatambua na kuwaenzi watu binafsi, taasisi na mashirika yaliojitokeza na kutoa mchango wao katika udhibiti wa UKIMWI,
Hapa nchini, mwaka huu maadhimisho yanafanyika kitaifa mkoani Mwanza katika viwanja vya Furahisha. Wadau wa kitaifa chini ya uratibu wa TACAIDS wamekamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya kutoa huduma muhimu kama vile Utoaji wa Taarifa na Habari mbalimbali za udhibiti wa VVU na UKIMWI kupitia Vyombo vya Habari, Vipeperushi, Mabango n.k. na Kutoa Ushauri Nasaha na Kupima VVU kwa hiari bila malipo kwa wiki nzima kuanzia tarahe 25 Novemba 2019. Shughuli hii itafanyika kwenye mabanda ya maonyesho na utoaji huduma na wataalamu wenye uzoefu.
Aidha, napenda kuwataarifu kuwa mikoa yote imeelekezwa kujipanga kuadhimisha siku hii. Natoa wito kwa wakuu wa mikoa wote kusimamia utekelezaji wa shughuli hii kwa kushirikiana na wadau wa kudhibiti VVU/UKIMWI walioko kwenye mikoa yao. Sambamba na wito huu nachukua fursa hii kuhamasisha wananchi katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na familia, sehemu za kazi, nyumba za ibada, shuleni, vyuoni na katika jumuia zetu mbalimbali kuadhimisha siku hii kwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma na kushiriki kwenye matukio mbalimbali yanayohusiana na maadhimisho haya.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu wa 2019 ni “JAMII NI CHACHU YA MABADILIKO; TUUNGANE KUPUNGUZA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU”. Maambukizi mapya ya VVU bado yanatokea nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa watu takribani 72,000 hupata maambukizi mapya nchini; hii ni sawa na wastani wa watu 6,000 kwa mwezi ama watu 200 kwa siku au watu 8 kwa saa. Hivyo, msisitizo mkubwa katika Kauli Mbiu ya mwaka huu ni ushiriki wa jamii kwenye kupunguza maambukizi mapya ya VVU kuanzia kwenye kuibua changamoto, kupanga mipango utekelezaji wa mipango na tathmini ya mipango hiyo. Imefahamika kuwa ushirikishwaji wa jamii una tija kubwa unapofanywa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya mahali husika. Jamii ndio yenye uwezo mkubwa wa ushawishi kwa mtu mmoja mmoja, familia na hata kwa viongozi wanaowawakilisha. Aidha, kauli mbiu hii inatilia mkazo kwenye kuunganisha nguvu katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU na hasa kwenye kundi la vijana. Takwimu zinaonyesha kuwa kundi la vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40 na hivyo kulifanya kundi hili kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU kuliko kundi lingine.
Hivyo Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha Wananchi, Makampuni na makundi mbalimbali ya jamii kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kudhibiti VVU/UKIMWI nchini ili kwa pamoja tuweze kuendana na mtazamo wa kimataifa wa kumaliza maambukizi mapya ya VVU ifikapo mwaka 2030.
Matukio yaliyopangwa kufanyika katika maadhimisho ya mwaka huu ni pamoja na:
Maonyesho ya Shughuli za Wadau wa kudhibiti VVU/UKIMWI nchini yatakayoanza tarehe 25 Novemba, 2019 yakijumuisha huduma mbalimbali na utoaji Elimu na Burudani kwa wananchi. Miongoni mwa huduma hizi ni ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa VVU, Upimaji wa Saratani ya Shingo ya Kizazi, Sukari, Uwiano wa Urefu na Uzito wa
- Mwili, na Elimu kupitia vikundi vya Sanaa na Burudani. Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma mbalimbali zitakazotolewa na wadau. Uzinduzi Rasmi wa wiki ya Maadhimisho haya utafanyika tarehe 25 Novemba 2019 kwenye viwanja vya Furahisha jijini Mwanza. Uzinduzi huu pia utaambatana na matembezi ya hisani kwa ajili ya kuutangaza na kuhamasisha uchangiaji wa Mfuko wa Udhamini wa Udhibiti wa UKIMWI (AIDS Trust Fund – ATF) yatakayoanzia kwenye jengo la Grand Hall, Nyamagana na kupokelewa uwanja wa Furahisha. Mgeni Rasmi katika Uzinduzi huu pamoja na matembezi ya hisani anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee Mh. Ummy Mwalimu (MB).
- Kutakuwa na maonyesho na utoaji wa huduma rafiki kwa vijana yatakayokuwa maalumu kwa ajili ya vijana kuanzia tarehe 25 hadi kilele chake tarehe 30 mwezi Novemba. Vijana wametengewa eneo maalumu litakalojulikana kama Kijiji cha Vijana ndani ya uwanja wa Furahisha. Vijana wote wa mkoa wa Mwanza na mikoa jirani wanakaribishwa. Aidha kutakuwa na utaratibu wa wadau kuwafikia vijana mahali walipo kama vile mialo ya samaki kwa ajili ya kupewa huduma za VVU/UKIMWI. Siku ya Kilele cha Maonyesho katika Kijiji cha Vijana (30/11/2019), Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu), Mh. Jenista Mhagama (MB).
- Kutakuwa na Kongamano la Kisayansi la Kitaifa la kutathmini Hali na mwelekeo wa udhibiti UKIMWI nchini litakalofanyika kati ya tarehe 28 hadi 29 Novemba 2019 jijini Mwanza katika ukumbi wa Mikutano wa Malaika Beach Resort. Kongamano hili litajadili mawasilisho ya utekelezaji wa afua za UKIMWI nchini. Wataalamu watabadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kujulishana mafanikio pamoja na kupanga namna ya kuboresha afua za kudhibiti VVU/UKIMWI nchini. Kongamano linakadiriwa kuhudhuriwa na wataalamu 150 kutoka Taasisi zinazotekeleza afua za VVU/UKIMWI, viongozi wa kisiasa pamoja na wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Mgeni Rasmi katika Kongamano hili anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee Mh. Dkt. Faustine Ndugulile (MB).
- Kilele caha maadhimisho kitakuwa tarehe Mosi Disemba 2019, kitakachofanyika kwa maandamano ya wadau wa kudhibiti VVU/UKIMWI na hotuba za viongozi wa kitaifa na kimataifa. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi wa Siku ya kilele cha maadhimisho. Hii itakuwa ni fursa nzuri ya uraghibishi ya kuelezea mikakati ya Serikali katika kusukuma mbele ajenda ya kutokomeza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Katika Maadhimisho haya tutakuwa na wageni waalikwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi katika ngazi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Mabalozi wa Nchi mbalimbali hapa nchini, wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Wadau wa Maendeleo, Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Dini, Asasi za Kiraia n.k.
Natoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika wiki ya maadhimisho haya nchini kote ili wapate huduma mbalimbali zitakazotolewa kama nilivyozitaja awali. Nawapongeza wadau wote waliochangia na kufanikisha maandalizi ya maadhimisho haya.