Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi USAID Tuhifadhi Maliasili, Doroth Nyoni akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari za mazingira walioshiriki katika mafunzo
Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru akiongoza mjadala.
Mwandishi Sidi Mgumia akichangia mada wakati wa mafunzo.
Waandaaji wa mafunzo (JET) wakifuatilia mjadala kwa karibu
…………………
NA SIDI MGUMIA, BAGAMOYO
Usawa wa kijinsia ni msingi muhimu kwa maendeleo endelevu, yenye athari mtambuka katika ukuaji wa kijamii na kiuchumi, afya na mazingira.
Kwa kusikitisha, wanawake na wasichana wanaendelea kuteseka na athari mbaya za usawa wa kijinsia licha yakuwepo kwa jitihada mbalimbali za kushughulikia masuala ya ukosefu wa usawa wa kijinsia.
Hali hiyo imechangia pakubwa wanawake wengi hasa waliopo kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi ama mapori ya akiba kujiona hawastahili kuwa walinzi wa maliasili hizo.
Kwa kuliona hilo Shirika la Misaada la Marekani kupitia mradi wake wa USAID Tuhifadhi Maliasili kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya usawa wa kijinsia kwenye usimamizi maliasili mbalimbali zikiwemo shoroba saba ambazo kwa sasa zimo ndani ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
Mradi huo unatekelezwa katika shoroba za Kwakuchinja, Amani Nilo, Udzungwa na Hifadhi ya Nyerere, Ruaha Rungwa na Katavi, Ruaha Rungwa na Inyonga na Kigosi Moyowosi- Burigi Chato.
Lengo kuu la mradi huo ambao umezingatia usawa wa kijinsia ni kusaidia makundi yote kushiriki katika shughuli za kiuchumi pia kuhakiksha unawaongezea uelewa wanawake katika kulinda shoroba ili ziendelee kuwa salama na kuwapa fursa wanyama kuhama kutoka eneo moja kwenda jengine kwa kupita kwenye njia zao za asili (shoroba).
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Doroth Nyoni ameyaeleza hayo juzi Februari 16, 2024 alipokuwa akiwasilisha mada kwa Waandishi wa Habari za Mazingira walioshiriki katika mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika, Bagamoyo mkoani Pwani.
Katika wasilisho lake Doroth alisisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia jinsia kwenye utekelezaji wa miradi ambayo inahusu uhifadhi na mazingira.
Doroth amesema katika ufuatiliaji na tathmini ambayo wamefanya wameona ushirikishwaji wa makundi yote wakiwemo wanawake, vijana, watoto na walemavu inasababisha rasilimali zote zinazopatikana kwenye hifadhi kuwa salama na kila mwanajamii kujiona ni mnufaika.
“Ili fursa zinazopatikana kwenye uhifadhi ziwe endelevu ni lazima ushirikishwaji wa kijinsia uzingatiwe, hatua hiyo inasaidia hifadhi kutunzwa na kuwa endelevu,” amesema.
Amesema Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umeshirikiana na wananchi waliopo karibu na shoroba ili kuhakikisha wananufaika na fursa zilizopo, ikiwemo kuanzisha vikoba, ujasiriamali na kupata tija nyengine.
Doroth amesema katika kusimamia misingi ya usawa wa kijinsia wamehakikisha makundi yote yanashiriki katika uongozi ili wawe sehemu ya maamuzi kuhusu rasilimali zao.
Taarifa za kitafiti zinaonesha wanawake na vijana ndio waathirika wakuu wa uharibifu wa mazingira, hivyo uamuzi wa kuzingatia usawa wa kijinsia utawanufaisha zaidi.
“Kampeni ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira ikiachwa kwa kundi moja, hatari itakuwa kubwa, sisi USAID Tuhifadhi Maliasili tumehakikisha jinsia inapewa nafasi.
“Kwenye shoroba ya Amani Nilo iliyopo wilayani Muheza mkoani Tanga tumefanya kampeni kuanzia ngazi ya shule za msingi, hali ambayo imewezesha hata watoto kutambua faida za hifadhi na hivyo kulizinda.
“Kwakuchinja mkoani Manyara kuna Programu ya Twende Porini nayo imefanikiwa kwa kuwa imejikita kwenye suala la kijinsia,” amesema.
Amesema kuwa kabla mradi huo haujaanza kushirikisha makundi yote, kulikuwa na hali ya baadhi makundi kuona wanatengwa, ila kwa utaratibu wa sasa hali imekuwa nzuri.
Alisema tayari wanawake 756 kati ya 1872 wameshafikiwa na mafunzo ikiwemo katika ngazi za juu za vijiji, ili kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye shuhuli za uhifadhi.
“Huu mradi malengo yake ni kuwajengea uwezo wanawake 1872, kwenye eneo la uongozi na mpaka kufikia sasa zaidi ya wanawake 756 wameshafikiwa,”alisema.
Aliongeza kuwa , “Kwenye baadhi ya shoroba tayari watu wameshaanza kunufaika na ardhi yao. Tumezingatia misingi ya kuwezesha uhifadhi ambao wananchi wananufaika na rasilimali hiyo ya shoroba. Mfano GFP amewezesha wakulima wa viungo wilayani Muheza kunufaika.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru amesema uamuzi wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kuzingatia misingi ya kijinsia unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa ndio mwelekeo wa dunia.
Dkt. Otaru amesema dunia kwa sasa inapigania usawa wa kijinsia, hivyo ni muhimu waandishi wa habari kueleza kwa kina kuhusu miradi ambayo inazingatia hayo.