Maji yaliyopoteza mwelekeo katika baadhi ya mito wilayani Mbarali yakiwa yameharibu mawasiliano baina ya vijiji kwa kukata sehemu za barabara kutokana na mvua zinazoendelea ukanda wa juu wa Uwanji eneo la Kitulo wilayani Makete na Mbeya na maji yake kutiririka kwa kasi kuelekea bonde la Ihefu kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.(Picha kwa hisani ya Halimashauri ya Wilaya ya Mbarali)
………
Na Joachim Nyambo, Mbeya
USAFIRI wa Powertiller, Bodaboda na kutembea kwa miguu vitatumika kama njia mbadala ya kufikisha huduma ya Chanjo ya Surua katika baadhi ya maeneo wilayani Mbarali mkoani Mbeya kufuatia miundombinu ya barabara kuharibiwa vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Denis Mwila yapo baadhi ya maeneo ambayo hayafikiki tena kwa usafiri wa gari kwakuwa maji ya mvua yameharibu miundombinu ya barabara na maeneo husika yana watoto wanaohitaji kupata huduma muhimu kama chanjo.
Mwila aliyasema hayo katika Kituo cha Afya cha Rujewa alipozindua Kampeni ya Chanjo ya Surua Lubela iliyoanza kutolewa jana nchini kote na itakamilika kesho kutwa ambapo kwa wilayani hapa jumla ya watoto 69, 343 ambao wana umri wa kuanzia miezi 9 hadi miaka 5 watapata chanjo hiyo.
Aliwasihi watumishi wa afya wanaohusika na chanjo kukubaliana na hali halisi ya kutumia aina hiyo ya usafiri pale itakapobidi kama usafiri mbadala kwa maeneo ambayo hayafikiki na magari.
“Inabidi kukubaliana na uhalisia uliopo. Hii ni kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya barabara hasa wakati huu wa mvua nyingi zinazoendelea kunyesha hapa Mbarali.” Alisisitiza Mwila.
“Inabidi watumishi watamie usafiri wa Powertiller , pikipiki kwa maana ya bodaboda , baiskeli na kutembea kwa miguu kwa yale maeneno yatakayokuwa na changamoto ya barabara.”
Aliitaja barabara ya Lihamile – Ikanutwa yenye urefu wa kilomita saba ikiwa na karavati nane kuwa miongoni mwa zilizoharibika vibaya na hazipitiki kwakuwa imekatika zaidi ya maeneo kumi hatua iliyomlazimu pia kuiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kusaidia ukarabati mkubwa wa barabara hiyo.
Kwa mujibu wa Mwila barabara hiyo inahitaji kiasi cha fedha kisichopungua Shilingi milioni 300 ili kuifanyia ukarabati na iweze kupitika tena na wananchi waendelee kupata huduma ya mawasiliano.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Dk. Ray Salandi alisema chanjo zilizopokelewa wilayani hapa ni 74,000 na chanjo ziliozidi zitakuwa kama ziada kwa watoto watakaoongezeka.
Dk Salandi alitoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto wa umri lengwa kuhakikisha wanapelekwa kuchanja lengo likiwa ni kuwalinda watoto hao dhidi ya magonjwa.
Baadhi ya wakazi wa vijiji vilivyopo maeneo ya pembezoni wameomba wadau wa usafiri wakiwemo madereva wa bodaboda na wamiliki wa Powertiller kuwapa msaada watoa huduma za chanjo pale watakapohitaji kuvifikia vijiji vilivyoharibikiwa miundombinu ya usafiri ili waweze kuwafikia wananchi na kuwapa huduma.
“Wakiwasafirisha watoa huduma kwa gharama kubwa wanaweza kukata tamaa ya kuvifikia vijiji ambavyo havifikiki kwa urahisi. Tunawaomba wenye vyombo vinavyoweza kufika waone kama wanasaidia kupelekaa chanjo kwa wananchi wenzao.”Alisema mkazi wa Kijiji cha Lyahamile, John Mattonya.
Historia inaonesha wilaya ya Mbarali ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto kwa kiasi kikubwa ya kuharibiwa kwa miundombinu ya usafiri kila mwaka zinapofululiza mvua nyingi hivyo ipo haja kwa kampeni muhimu kufanyika nyakati za kiangazi ili kuepuka kukwama zoezi husika.