Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila, akizungumza wakati akifungua semina ya siku tatu iliyoandaliwa na BoT kwa waandishi wa habari kuhusu majukumu yake, pamoja na mfumo mpya wa uandaaji na utekelezaji wa sera mpya ya fedha kwa kutumia Riba ya Benki Kuu ulioanza kutumika mwezi Januari 2024. Semina hiyo inafanyika katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya BoT Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024.
…………………………….
Na John Bukuku, Zanzibar
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari juu ya mfumo mpya wa uandaaji na utekelezaji wa sera mpya ya fedha utakaosaidia kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi.
“Hii ni kwa sababu mfumo huu utawezesha Benki Kuu ya Tanzania kurekebisha riba kulingana na hali ya uchumi na kuhakikisha kwamba kuna usawa kati ya mahitaji na usambazaji wa fedha,” amesema Naibu Gavana wa BoT (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila, wakati anafungua semina hiyo inayofanyika katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya BoT Zanzibar kuanzia Februari 14 hadi 16, 2024.
Amesema mfumo huo pia utasaidia kuzuia kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, ambazo zinaweza kupunguza nguvu ya ununuzi wa wananchi na kudhoofisha ukuaji wa uchumi.
Pamoja na mafunzo kuhusu sera ya fedha, washiriki wa semina hiyo kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, watajifunza kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, ikiwemo masuala ya mikopo; namna Benki Kuu inavyomlinda mtumiaji wa huduma za fedha; na faida za kutumia mifumo mbadala ya malipo badala ya pesa taslimu.
Akizungumzia kuhusu huduma ndogo za fedha, Dkt. Kayandabila amesema Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2018 ili kurasimisha shughuli hizo.
Ameeleza kuwa siku za karibuni kumekuwepo na malalamiko kwa watu kuwa riba ziko juu hadi kufikia hatua ya baadhi kupewa majina ya mikopo mbalimbali kama kausha damu.
“Kumbukeni mikopo hii inasaidia sana watu, kuipa majina kama hayo inakuwa siyo jambo zuri kwani mikopo hii inasaidia watu kutatua mahitaji yao muhimu, ikiwemo kusomesha watoto”, amesema Dkt. Kayandabila.
Ameeleza kuwa kwa sasa BoT ina kurugenzi inayoshughulikia malalamiko ya walaji wa huduma za kifedha na kwamba watu wakipeleka malalamiko yao huko yanashughulikiwa ipasavyo.
Kuhusu matumizi ya njia mbadala za malipo badala ya pesa taslimu, Naibu Gavana amesema: “Watu wanakwenda kwenye taasisi za fedha wanatoa fedha nyingi wanaweka kwenye begi kitu ambacho siyo salama, hivyo lazima tuanze kutumia mifumo ya kuhamisha fedha ili kuepukana na changomoto za kuibiwa”, amesema Dkt. Kayandabila.
Caption: Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Yamungu Kayandabila akimsikiliza Meneja Mawasiliano wa BoT, Bi. Victoria Msina, wakati akitoa utambulisho kwa waandishi wa habari wanaoshiriki katika mafunzo kuhusu majukumu ya BoT, ukiwemo mfumo mpya wa uandaaji na utekelezaji wa sera mpya ya fedha kwa kutumia Riba ya Benki Kuu ulioanza kutumika mwezi Januari 2024. Semina hiyo inafanyika katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya BoT Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa BoT tawi la Zanzibar Masoud Suleiman.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Yamungu Kayandabila akimsikiliza Meneja Mawasiliano wa BoT Bi. Vick Msina wakati akitoa utambulisho kwa waaandishi wa habari wanaoshiriki mafunzo ya siku tatu juu ya mfumo mpya wa uandaaji na utekelezaji wa sera mpya ya fedha utakao saidia kupunguza changamoto ya wizi kwa wananchi yanayofanyika katika tawi la BoT Zanzibar kuanzia Februari 14-16, 2024. kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa BoT tawi la Zanzibar Masoud Suleiman
Kaimu Mkurugenzi wa BoT tawi la Zanzibar Masoud Suleiman akifafanua jambo kwa waandishi wa habari katika mafunzo hayo.
Wawasilishaji wa Mada katika mafunzo hayo kutoka kulia ni John Rhodes Mero Meneja Msaidizi Uchambuzi wa Sera ya Fedha BoT na Dkt. Lusajo Mwankemwa Meneja Msaidizi Utafiti BoT.
Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo Salma Said kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW Ujerumani akifafanua mambo kadhaa katika mafunzo hayo kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa BoT tawi la Zanzibar Masoud Suleiman.
Picha zikionesha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari pamoja na maofisa kutoka Benki Kuu ya Tanzania BoT wakiwa katika semina hiyo .