Na. Anangisye Mwateba-Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii imekamilisha mchakato wa kufanya tathmini ya malipo ya kifuta jasho/ machozi ambapo kiasi cha shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Sita zinatakiwa kulipwa kupitia Wizara ya Fedha.
Haya yamebainika wakati Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula akijibu swali la Mhe. Dkt. David Mathayo David(Mb) aliyetaka kujua lini Serikali itafanya mapitio ya Sheria na Kanuni za fidia kwa waathirika wa wanyamapori ili kulipa fidia ya gharama halisi tofauti na sasa.
Aidha, Wizara imekamilisha mapitio ya Kanuni za Kifuta Jasho/Machozi na kuiwasilisha Wizara ya Fedha ili kuona uwezekano wa kuongeza viwango hivyo.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa kwa sasa Wizara ya Fedha inafanya tathmini ili kuona athari za kiuchumi na uwezo wa nchi kutekeleza suala hilo.
“Wizara imekuwa ikilipa kifuta jasho/ machozi kama mkono wa pole au faraja kwa wananchi wanaopata madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu. Malipo hayo yamekuwa yakifanyika kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho/Machozi za mwaka 2011 na kwa kadri ya upatikanaji wa fedha” alisema Mhe. Kitandula.
Pia, Mhe. Kitandula aliongeza kuwa wizara inafahamu kumekuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa malipo hayo, sababu kubwa ikiwa ni ulazima wa kufanyika kwa tathimini ya kina inayolazimu kwenda uwandani ili kuhakiki na kujiridhisha kiwango cha uharibifu au madhara yaliyojitokeza na fidia stahiki inayopaswa kutolewa.