Mratibu Miradi wa Shirika lisilo la kiserikali la Wanawake Amkeni ‘Women Wake Up’ (WOWAP),Nasra Suleiman, akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mangda kwenye mkutano wa hadhara kuhusu mila potofu na madhara ya ukeketaji kwa mtoto wa kike uliofanyika jana Kata ya Msange Halmashauri ya Wilaya ya Singida DC.
Mzee Kinusa Muna akizungumza kwenye mkutano huo.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri hiyo, Felix Maigo, akizungumza kwenye mkutano huo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago. akihamasisha jamii kuondokana na dhana ya ukeketaji kwenye mkutano huo.
Wanakwaya wa kikundi cha sanaa cha wanawake wa Kijiji cha Mangda wakitoa burudani.
Klabu ya Haki za Binadamu inayoundwa na kundi la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Madasenga, wakiimba shairi maalumu lenye ujumbe wa kutokomeza ukeketaji kwenye mkutano huo.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondary Madasenga wakiimba kwenye mkutano huo.
Wananchi wa Kijiji cha Mangda wakiwa kwenye mkutano huo.
Mtendaji wa Kata ya Msange, Samwel Nhango, akizungumza kwenye mkutano huo.
Baadhi ya Maofisa wa Shirika la WOWAP wakifurahia moja ya igizo lenye ujumbe maalumu wa kupinga ukeketaji kwa mtoto wa kike.
*********************************
Na Mwandishi Wetu, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Wanawake Amkeni ‘Women Wake Up’ (WOWAP), limetoa wito kwa watanzania kuungana pamoja katika kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili kwa mtoto wa kike, hususan masuala ya ukeketaji ambayo bado hufanyika kwa siri sana kwa baadhi ya maeneo, huku mtindo unaotumiwa kwa sasa ukigeukia zaidi watoto wachanga hali inayohatarisha mustakabali mzima wa ukuaji wa mtoto kiafya, kimwili na kiakili.
Akizungumza mbele ya wakazi wa Kijiji cha Mangda, Kata ya Msange, Singida DC, mkoani hapa, kwenye mkutano wa hadhara ulioambatana na burudani za kwaya, mashairi na maigizo yenye ujumbe wa ‘KATAA NA TOKOMEZA UKEKETAJI KWA MTOTO WA KIKE,’ Mratibu Miradi kutoka WOWAP unaofadhiliwa na Women Action Against FGM (WAAF JAPAN), Nasra Suleiman, alisema ukatili huo wa kutisha unachangiwa zaidi na mambo ya kiimani anayoaminishwa mtu, sambamba na mila na desturi potofu zilizopitwa na wakati.
“Nichukue nafasi hii kuwasihi sana viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wazazi, Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla tushikamane ili kwa pamoja tuweze kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa watoto wetu hawa wa kike,” alisema Suleiman.
Alisema kinachosikitisha zaidi ukatili huo kwa sasa unaelekezwa zaidi kwa watoto wachanga na hufanyika kwa siri sana kwa wahusika kuogopa mkondo wa sheria, hali inayopelekea ugumu wa kubaini vitendo hivyo mpaka labda pale madhara makubwa au hali ya ugonjwa inapojitokeza.
Alibainisha kwamba pamoja na mambo mengine, madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike huweza kusababisha vifo kutokana na mwathirika wa tukio hilo kutokwa na damu nyingi, maambukizo ya magonjwa na hasa UKIMWI kutokana na vifaa vinavyotumika kwa ukeketaji kutokuwa safi na salama, maumivu makali wakati wa kujamiiana na kujifungua, na madhara ya kimwili na kisaikolojia.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Singida, Shukrani Mbago, alisema azma iliyopo kama mkoa ni kuhakikisha wanatokomeza kabisa vitendo vya ukeketaji ndani ya maeneo yote ya mkoa huo na wahusika watakaobainika kufanya vitendo hivyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Mbago alisema haikubaliki hata kidogo kuona vitendo hivyo vikiendelea, huku akiwasihi wanasingida wote kushikamana na kuwa mabalozi wazuri wa kampeni hiyo- kwa kila mmoja kutamka neno ‘acha’ ili kwa pamoja kuweza kumaliza kabisa ukatili huo mkubwa anaofanyiwa mtoto wa kike
Alisema serikali mkoani hapa kwa kushirikiana na WOWAP wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu dhidi ya mila na desturi potofu zinazochochea vitendo hivyo vya ukeketaji… na kuwasihi wadau wengine kuunganisha nguvu katika kuhamasisha na kutoa elimu stahiki ambavyo vitaleta mageuzi chanya kwenye kampeni hiyo, na hasa kwenye eneo la kuwawezesha ndugu wa karibu na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufichua taarifa zenye viashiria vyovyote vya matendo ya ukeketaji kwa mtoto wa kike.
Mbago alisema kwa mujibu wa takwimu za kitafiti, mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa mitano kitaifa ambayo masuala hayo ya ukeketaji yameonyesha kushamiri. Takwimu zinaonyesha asilimia 31 ya wanawake wa mkoa huo wamekumbwa na kadhia hiyo ya kufanyiwa ukeketaji, jambo ambalo alisisitiza sio la kujivunia hata kidogo, na kwamba jamii inapaswa kukataa hali hiyo na kubadilika.
Katika mkutano huo Klabu ya Haki za Binadamu inayoundwa na kundi la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Madasenga, na kikundi cha sanaa cha wanawake cha Mangda ni miongoni mwa washiriki waliochagiza kampeni hiyo na kuibua hamasa ya aina yake na kupelekea wengi miongoni mwa waliohudhuria kampeni hiyo kuazimia kuwa mabalozi waaminifu dhidi ya mila kandamizi na matendo ya ukatili ikiwemo ukeketaji kwa mtoto wa kike.