Home Mchanganyiko RC GAGUTI  AWACHUKULIA HATUA WASIMAMIZI WA MIRADI YA UKARABATI WA SHULE KONGWE...

RC GAGUTI  AWACHUKULIA HATUA WASIMAMIZI WA MIRADI YA UKARABATI WA SHULE KONGWE KWA UZEMBE.

0

******************************************

Na: Silvia Mchuruza.
Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti amwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Revocatus Malimi kuwaweka chini ya ulinzi wasimamizi wa miradi ya ukarabati wa Shule kongwe katika Manispaa ya Bukoba baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo na kutoridhishwa na kasi ya maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo wakati Serikali ilishatoa fedha zote za ukarabati kila shule.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alichukua hatua hiyo Septemba 21, 2019 wakati wa ziara yake Manispaa ya Bukoba katika Shule kongwe za Kahororo, Rugambwa, Kagemu na Bukoba ambazo kwa pamoja zilipewa jumla ya shilingi bilioni 2,595,890,485.33 na Serikali kufanya ukarabati wa majengo ili kuzirejesha shule hizo katika hali nzuri lakini pamoja fedha hizo kuingizwa katika kila akaunti ya shule husika ukarabati umechukua muda mrefu au kuendelea kwa kusuasua na kupitiliza muda uliotolewa na Serikali kukamilika.
Baada ya kufika katika Shule ya Sekondari Kahororo na kutoridhishwa na ukarabati unaoendelea kwa kudorora pia kutoridhishwa na maelezo ya mkandarasi ambaye ni Mzinga Holding Company alimwelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Revocatus Malimi kuwaweka chini ya ulinzi Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Marck Ogambage kwa uzembe wa usimamizi pamoja na Mhandisi Festo Talimo wa Mzinga kwa kufanya kazi kwa uzembe lakini pia Afisa Manunuzi wa Manispaa ya Bukoba Batreth Rwiguza kwa kufanya kizembe mchakato wa manunuzi ya vifaa vya ujenzi.
Wengine waliochukuliwa hatua kwa uzembe huo ni pamoja na Kaimu Mhandisi wa Manispaa ya Bukoba George Geofrey   kutosimamia ipasavyo ukarabatihuo aidha,  katika Shule ya Sekondari Bukoba Kaimu Mkuu wa Shule Mwalimu Siasa Phocus pia alichukuliwa hatua kwa kuzembea kusimamia ukarabati wa shule hiyo huku zaidi ya milioni 900 zikiwa zimeishatumika kati ya Shilingi bilioni 1,481,701,194.33 zilizotolewa na Serikali kuhakikisha shule hiyo inarudi katika hali nzuri.
Shule ya Sekondari Kagemu ilipewa na Serikali Shilingi milioni 152,000,000 tayari muda wa ukarabati umeisha na zimelipwa milioni 49,485,277.22 Shule ya Sekondari Kahororo ilipewa na Serikali shilingi milioni 893,883,994 kati ya hizo zimetumika  shilingi milioni 297,966,594.96 muda wa ukarabati ukiwa umeisha bila kazi kukamilika. Shule ya Sekondari Rugambwa ilipewa shilingi milioni 872,800,297 na zilizotumika ni shilingi milioni 275,125,889.25 ambapo muda wa ukarabati ukiwa umeisha.
Mradi wa Barabara 
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti alitembelea na kukagua mradi wa barabara wa kilometa tano unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kujengwa katika Manispaa ya Bukoba wenye thamani ya shilingi bilioni 7.3 ambapo  alimweleza mkandarasi huyo kuhakikisha mradi huo unakamilika mapema  ikiwa mradi huo unaongozwa na Kampuni ya JASCO Building and Civil Engineering Contractors ya Jijini Mwanza
Mwisho Mhe. Gaguti alimweleza Mkandarasi huyo wa  Kampuni ya JASCO kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa .