NA
K-VIS BLOG/Khalfan Said, Songea
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewahimiza waajiri nchini
kujisajili na kutoa taarifa za ajira za wafanyakazi wao kwenye Mfuko wa Fidia
kwa Wafanyakazi (WCF) ili kulinda haki za wafanyakazi hao pindi wanapopatwa na
majanga wakiwa kazini.
Mhe. Jaji Siyani
ameyasema hayo mjini Songea wakati akifungua Kikao Kazi cha Mafunzo kuhusu
sheria ya fidia kwa wafanyakazi kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini, watendaji wa mahakama na Tume ya Usuluhishi
na Uamuzi (CMA) kilichoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
“Pamoja na
uwepo wa sheria inayowabana waajiri wanaoshindwa kuwasajili wafanyakazi wao WCF
lakini bado kuna waajiri ambao hawatoi taarifa za ajira za wafanyakazi wao na
hivyo kuuweka mfuko katika nafasi ngumu ya kutekeleza majukumu yake,”
amefafanua.
Jaji Siyani
ametoa mfano wa kisa cha mfanyakazi mmoja aliyekuwa akifanya kazi kwenye
kampuni moja ya ujenzi mkoani Lindi ambaye aliumia akiwa kazini na kupelekea
kupoteza baadhi ya viungo vyake na
kumsababishia ulemavu wa kudumu kwa zaidi ya asilimia 75 lakini alikosa vigezo
vya kupata fidia kwa kuwa mwajiri wake hakuwa amejisajili na kuwasilisha
michango WCF kwa mujibu wa sheria.
“Licha ya kijana
huyo kufanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili lakini taarifa zake hazikuwepo WCF
na hivyo kukosa haki ya kupata fidia yoyote” ameeleza Jaji Siyani; na kuongeza
kuwa iwapo zingekuwepo taarifa za mfanyakazi huyo, bila shaka angepata fidia
bora zaidi ya ile iliyotokana na majadiliano na maridhiano na mwajiri wake.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma,
amesema Mahakama ya Tanzania ni wadau muhimu wa Mfuko huo katika utekelezaji wa
majukumu yake kwa kuwa Mfuko unategemea maamuzi mbalimbali ya mahakama katika
utekelezaji wake wa majukumu ikiwemo maamuzi ya kesi za mirathi.
Dkt. Mduma
amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya
Serikali yanayozitaka taasisi zake kuhakikisha zinashirikiana kwa
karibu kwa dhumuni la kuongeza tija na huduma bora kwa wananchi.
Pia, mafunzo
hayo yanatoa fursa ya kubadilishana uzoefu baina ya wataalam wa Mahakama na WCF
kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa ambapo washiriki wanaweza kuja na
mapendekezo yatakayoboresha utendaji kazi wa Mfuko huo.
“Ni
matarajio yangu kuwa mafunzo haya yataleta manufaa makubwa kwa pande zote
mbili, ikiwemo kuimarisha mahusiano kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi
na kuchangia kukuza uchumi wa nchi yetu na hasa kupunguza umasikini kwa wafanyakazi
watakaopata majanga yanayotokana na kazi zao,” amesisitiza Dkt. Mduma.
Mafunzo hayo
ambayo ni ya awamu ya nne yamewaleta pamoja washiriki kutoka mikoa ya Ruvuma,
Mtwara, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa ambapo miongoni mwa mada zinazotarajiwa
kuwasilishwa ni kuhusu sheria ya fidia kwa wafanyakazi, taratibu za
uwasilishaji na ushughulikiaji wa madai ya fidia kwa wafanyakazi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohammed Siyani,
akizungumza kwenye kikao kazi cha Mafunzo ya Uelimishaji kwa Waheshimiwa Majaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kilichoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi (WCF), mjini Songea, Februari 9, 2024.
JAJI
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohammed Siyani
(katikati), akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma (kulia) na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha, akizungumza
kwenye kikao kazi cha Mafunzo ya Uelimishaji kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kilichoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi
(WCF), mjini Songea, Februari 9, 2024.
Mkurugenzi
Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma (aliyesimama kushoto), akizunguzma na Waheshimiwa Majaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) mjini Songea, Februari 9, 2024. Pamoja nae kutoka kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohammed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.
Baadhi
ya washiriki
Baadhi
ya washiriki
Baadhi
ya washiriki
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohammed Siyani (kushoto),
akikabidhiwa vitendea kazi vya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutoka kwa
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohammed Siyani (katikati)
akipeana mikono na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi,
Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kushoto) huku Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma
(kulia) na Jaji Mfawidhi Mahakama KUU Knada ya Songea, Mhe. Mhe.
James Karayemaha wakishihudia