Tanzania na Poland zimejadiliana na kukubaliana kushirikiana katika sekta za kimkakati ambazo zitawezesha kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Poland Andrzej Duda wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Duda yupo Tanzania kwa ziara ya Kitaifa ya siku mbili ambapo amepegiwa mizinga 21 na kufanya mazungumzo ya ndani na Rais Samia na wasaidizi wao kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Akizungumza na waandishi wa habari Rais Samia kabla ya kumkaribisha mgeni wake, amesema mazungumzo yao yalijikita katika sekta za afya, kilimo, utalii, uwekezaji, biashara, uchumi wa buluu, teknolojia ya habari na mawasiliano, viwanda, uzalishaji, nishati, gesi asilia na madini.
Amesema nchi hizo zimekuwa zikishirikiana kwa zaidi ya miaka 62 sasa, hivyo ujio wa Rais Duda unafungua ukurasa mpya ambao utawezesha sekta hizo za kimkakati kuimarika zaidi na kuwa na tija kwa pande zote.
Rais Samia amesema Poland imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania ambapo watalii 41,000 wamekuja nchini, huku katika kipindi cha mwezi Januari 2024 watalii 6,000 kutoka Poland wamekuja.
“Tumezungumza namna ambavyo ushirikiano wetu unaweza kuwa na tija hasa katika sekta ya kimkakati ambazo zitakuza uchumi kwa haraka, ambapo kwa kuanza timu ya wataalam imeelekezwa kuchukua hatua zitakazowezesha kuanza kwa safari za moja kwa moja kati Tanzania na Poland,” amesema.
Rais Samia amesema safari hizo zitachochea zaidi utalii pamoja na biashara kwa kuwa Poland ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa watalii na uchumi wake ukiwa wa 21 duniani.
Aidha, Rais Samia amewakaribisha wawekezaji kutoka Poland kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye sekta ya utalii hususani ujenzi wa hoteli.
Rais Samia amesema pia Tanzania na Poland zitaendelea kushirikiana kwenye sekta ya elimu na afya ambapo Watanzania watapata fursa ya kujifunza zaidi.
“Poland ipo tayari kutoa bima kwa benki za biashara kupitia Wakala wa Mikopo wa Usafirishaji kwa ajili ya utekelezaji mradi wa reli ya kisasa kwa vipande vya Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Isaka,” amesema.
Naye Rais Duda amesema nchi yake itahakikisha sekta zote ambazo wamejadiliana utekelezaji unafanyika kwa haraka ili dhamira ya kukuza uchumi iweze kutimia.
Rais Duda amesema pia wanatoa fursa kwa wanafunzi wa Kitanzani kwenda Poland kusoma masuala ya teknolojia na mabadiliko ya tabianchi.
“Sisi tutakaporudi nyumbani tutahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza Tanzania, lakini pia tunaamini elimu kuhusu TEHAMA na madini itasaidia kukuza uchumi,” amesema.
Aidha, Rais Duda amemualika Rais Samia na wasaidizi wake kufanya ziara ya kitaifa nchini Poland ambapo wataweza kuzungumza zaidi kuhusu ushirikiano wao, ambapo Rais Samia amekubali mwaliko huo.