Na Issa Mwadangala
Wakati dunia ikiendelea kuhamasisha Usawa wa kijinsia kupitia Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030) lengo namba 5 pamoja na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa, Wanawake wa Majeshi ya Ulinzi nchini wamefanya mkutano wa kujadili namna watakavyoshiriki katika siku ya Kimataifa ya Wanamke Duniani (International Women’s Day ) inayoadhimishwa 8 Machi Kila Mwaka.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF- NET) Wilaya ya Mbozi Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP. VERONICA MYOVELA amesema wanawake wa Majeshi hawawezi kuwa nje ya maadhimisho ya siku hiyo. Hivyo wanapaswa kuonesha ushiriki wao kikamilifu kama wanavyoshiriki wanawake wengine duniani kote.
Hata hivyo amewataka wanawake hao kutoa elimu kuhusu umuhimu wa siku hiyo ambayo inalenga kuunga mkono harakati zinazofanywa na mashirika mbalimbali ya kimataifa katika kumuwezesha mwanamke kwenye nafasi za uongozi, uchumi na maamuzi.
Mkutano huo uliofanyika Februari 09, 2024 ulishirikisha wanawake wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji ambapo kauli mbiu ya kimataifa katika siku ya Mwanamke mwaka huu ni “WEKEZA KWA WANAWAKE: KUHARAKISHA MAENDELEO”