Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema serikali kupitia wizara ya afya imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vya kidigitali ili kuwezesha na kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ameyasema hayo tarehe 8 Februari, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utoaji wa huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga na Kituo cha Afya Mazwi katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Dkt. Magembe amesema kwa mara ya kwanza mkoani humu Serikali imeweza kununua mashine mpya ya kisasa CT-scan na tangu kufungwa kwa mashine hiyo mwezi Desemba 2022 hadi leo imeweza kuhudumia wagonjwa takribani 96.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa ili watanzania wapate huduma bora, kwa mara ya kwanza katika historia ya mkoa huu ameweza kununua mashine mpya ya kidigitali ya CT- Scan ambayo imeanza kuwahudumia wagonjwa mbalimbali kama vile wahanga wa ajali, wenye matatizo ya Uti wa Mgongo, kiharusi na magonjwa mengine ya viungo vya ndani hadi kufika leo wamefika takribani wagonjwa 96” Amesema Dkt. Magembe.
Amesema kuwa Kwa sasa Hospitali hiyo inawapiga picha wa 4 ila bado hakuna msomaji na hivyo picha hizi zinatumwa kidigitali kwenda Hospitali ya Kanda Mbeya na majibu yanarudi ndani ya masaa 2 hadi 6, jambo ambalo limewezeshwa na uamuzi wa Mhe Rais Dkt Samia baada ya kununua mashine za kidigitali kama sehemu ya mkakati mmoja wapo wa kukabiliana na upungufu wa watumishi nchini.
“Sasa hivi duniani unaweza kufanyiwa hadi upasuji na bingwa au bobezi aliyepo nchi nyingine wakati mgonjwa yupo nchi nyingine, mgonjwa anakuwa kwenye kitanda cha upasuaji unaendelea na wataalamu wawili wanawasiliana bila shida yoyote, hii ndio sayansi katika tiba kwa kutumia mifumo ya TEHAMA (Telemedicine) ambapo kwa hapa nchini tumepiga hatua kwa kuwa na hospitali 16 zenye aina hii ya mtandao.” Amesema
Pia Dkt. Magembe alipata wasaa wa kutembelea na kuzungumza na wagonjwa waliokuja kupata huduma hospitalini hapo na kuwapa elimu juu ya faida za kujiunga na mfuko wa taifa wa Bima kwa wote na kuwaeleza njia wanazoweza kutumia ili kuwawezesha kutoa changamoto au mrejesho kwa Hospitali au vituo vya afya wanapoona hawaridhiki na huduma zinazotolewa
Kwa upande mwingine Dkt. Magembe aliwasisitiza watumishi kuwapa wagonjwa taarifa zote ikiwemo kuwaonyesha namba za simu zilizobandikwa kwenye na kujitambulisha kwa wagonjwa kabla ya kuanza kuwahudumia na kuwaambia wagonjwa taarifa muhimu zinazohusu matibabu yao ikiwemo vipimo, dawa wanazopewa na zinafanya kazi gani.
Akitoa taarifa, Mteknolojia wa Mionzi Bi. Lutfia Mohmoud Khamis alimuonyesha Naibu Katibu Mkuu Data base yenye wagonjwa 96 ambao wameshapatiwa huduma, ambapo kabla ya mashine hii wagonjwa walikuwa wanaenda Hospitali ya Kanda Mbeya yenye umbali wa kilometa 340 kupata huduma hii na kumshukuru Mhe Rais Dkt Samiah Suluhu Hassan kwa mashine hii ambayo imeleta mapinduzi makubwa kwenye tiba
“Wakati nahamia hapa palikuwa na Xray moja tena ya ki-analojia na imechoka, leo siamini Rukwa kuna CT-scan, X-ray mbili za kidijitali yaani nafurahia kazi yangu nimshukuru sana Rais Dkt Samia uwekezaji huu mkubwa alioufanya katika hospitali yetu”. Amesema Bi Lutfia.