Na. Projestus Binamungu – OR TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale amewataka Wakurugenzi wa Wizara za Sekta mbalimbali na Taasisi za Umma kuwa na mkakati mahususi wa kuwezesha utekelezaji wa mipango na bajeti za kisekta ili iwe na tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Bw. Mtwale ametoa wito huo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikaokazi cha kujadili mipango na bajeti za wizara za kisekta kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichowahusisha wakurugenzi wa wizara, taasisi pamoja wataalam.
Bw. Mtwale amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kujadiliana kuhusu maandalizi ya mipango na bajeti za wizara za kisekta za mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuweka mazingira bora ya utekelezaji wake kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa na ustawi wa jamii.
“Mipango na bajeti za utekelezaji wa kisekta inapaswa kuwekewa mkakati mahususi wa pamoja ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wake katika ngazi za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa,” Bw. Mtwale amesisitiza.
Bw. Mtwale ameanisha kuwa, utelezaji wa miradi na shughuli za kisekta katika mamlaka za serikali za mitaa baadhi ya maeneo umekuwa na changamoto kwasababu ya kutokuwa na uratibu mzuri katika maandalizi na utekelezaji wake hivyo amewata washiriki kuweka utaratibu wa kutatua changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa, anatarajia kikao kazi hicho kitatoa mwelekeo sahihi wa namna bora ya kuratibu na kutekeleza shughuli mbalimbali za kisekta hususani katika maandalizi ya mipango na bajeti za kisekta katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuwezesha utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka na utekelezaji wa ilani ya CCM.
Amesisitiza kuwa, OR-TAMISEMI itahakikisha inaendelea kushirikiana na wizara za kisekta ili kuwezesha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa na Serikali ili kuongeza kasi ya utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.