Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Misechela kata ya Misechela wilayani Tunduru,wakipata huduma ya maji katika moja ya visima vinavyotumia pampu ya mkono,hata hivyo tayari serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA)imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji ya bomba ambao pindi utakapokamilika utatatua changamoto ya maji katika kijiji hicho na kijiji jirani cha Liwanga.
WAKAZI wa vijiji viwili vya Misechela na Liwanga kaya Misechela wilayani Tunduru,wanakwenda kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya serikali kutoa Sh.bilioni 3,020,150,910.00 ili kutekeleza mradi wa maji utakaowanufaisha wakazi zaidi ya 9,050 wa vijiji hivyo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Mhandisi Maua Mgallah alisema,ujenzi wa mradi huo umeanza tangu mwezi Novemba 2023 na unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Novemba 2024 na unatekelezwa kwa fedha za serikali kuu kupitia program maalum ya malipo kwa matokeo(PforR).
Alitaja kazi zilizopangwa kufanyika katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 300,000,ujenzi wa tenki la chini la lita 75,000,ujenzi wa banio,uchimbaji wa mitaro na kulaza mabomba umbali wa mita 24,890 na kujenga vituo 28 vya kuchotea maji.
Aidha,kazi nyingine zinazofanyika ni kujenga nyumba ya mitambo,ufungaji wa umeme jua(solar power)ufungaji wa pampu na ujenzi wa ofisi ya jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO).
Mgallah alisema,katika awamu ya kwanza kazi zilizoanza kutekelezwa ni ujenzi wa tenki,nyumba ya mitambo,kuchimba mitaro urefu wa kilomita 4 na ofisi ya CBWSO ambapo ujenzi vituo vya kuchotea maji, kufunga umeme na mashine ya kusukuma maji bado haujaanza.
Alisema, mradi huo utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 2.69 kutoka asilimia 70.01 ya sasa na hivyo kufikia asilimia 72.7 katika wilaya hiyo.
Pia alisema,serikali imetoa Sh.milioni 70 zilizotumika kutekeleza mradi wa kusambaza maji safi na salama kwa wakazi wapatao 3,456 wa kijiji cha Masonya kata ya Masonya mradi uliotekelezwa na wataalam wa ndani.
Alitaja kazi zilizofanyika katika utekelezaji wa mradi huo ni ujenzi wa mnara wa mita 6 kwa ajili ya kubeba matenki mawili ya plastiki,ununuzi na ufungaji wa matenki yenye ukubwa wa lita 10,000 kila moja,kuchimba mitaro na kufunga bomba umbali wa mita 7,080 na kujenga vituo 6 vya kuchotea maji.
Diwani wa kata ya Misechela Zuber Binamu,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi zilizowezesha kuanza kwa ujenzi wa mradi huo ambao utakapokamilika utamaliza kabisa changamoto ya maji katika vijiji vya Misechela na Liwanga.
Alisema,kwa muda mrefu sasa wananchi hasa wanawake wa vijiji hivyo wanateseka kwa kuamka usiku wa manane na kutembea umbali mrefu hadi mto Ruvuma kwenda kuchota maji.
Mwenyekiti wa kijiji cha Misechela Said Msonjela alisema,katika kijiji hicho changamoto ya maji safi na salama ni kubwa na ameiomba serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira(Ruwasa)kukamilisha ujenzi wa mradi haraka ili waweze kuondokana na adha ya maji.
Alisema ni matumaini yao kwamba, mradi huo utakapokamilika utachochea sana maendeleo ya mtu mmoja mmoja na wilaya ya Tunduru,kwani wananchi watapa muda mwingi wa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kutumia muda wao kwenda kuchota maji.
Mkazi wa kijiji hicho Adan Sibati alisema,katika kijiji hicho kuna maji ya kupampu kwa mkono,lakini kutokana na idadi ya watu waliofika kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo za ufugaji na biashara maji hayo hayatoshelezi.