*********************************
Na Ahmed Mahmoud Arusha
JESHI la polisi mkoa wa Arusha linawashikilia watu kadhaa akiwemo Mwalimu wa shule ya Msingi kwa kukutwa na Bunduki AK 47 anayoitumia katika matukio ya uhalifu ikiwemo ujangili na biashara ya silaha,
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, amemtaja Mwalimu huyo kuwa ni Solomoni Letato Kipuker miaka (30 ) ambae ni mwalimu wa shule ya msingi Naan, iliyopo kata ya Engusero sambu tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro amekamatwa Juni 2 mwaka huu akiwa na bunduki pamoja na magazine yenye risasi tano.
Amesema Kuwa mwalimu huyo amekamatwa kwa ushirikiano wa wa kikosi kazi kambambe na Jasiri dhidi ya ujangili na uhalifu wa silaha za moto kanda ya Ziwa chini ya uwezeshaji wa Tanapa kwa tuhuma za kuhusika na ujambazi,kukamatwa na nyara za serikali.
Amesema mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa wafanyabiashara haramu ya uingizaji silaha za moto nchini pamoja na biashara ya nyara za serikali hasa meno ya Tembo na Pembe za Faru na shughuli zingine za ujangili na Ujambazi na utekaji watalii na wananchi
Kamanda Shana,amesema jeshi la polisi limefanikiwa kukamata silaha moja ya AK 47 iliyotelekezwa kwenye ofisi ya kijiji cha Mbukeni kata ya Arash tarafa ya Loliondo, baada ya kuwepo kwa taarifa za Kiintelejenisia ikiwa na risasi moja na watuhumiwa wanatafutwa.
Amesema mara baada ya kumhoji mtuhumiwa huyo alikiri kujihusisha na vitendo hivyo kwa kushirikiana na watuhumiwa wengine ambao wametoroka na wanatafuta na pia silaha hiyo imekuwa ikitumika kwenye mapigano ya kikabila kati ya Maasai, Wasonjo na Watemi, wilayani Ngorongoro.
Amesema jeshi la polisi linampongeza Kamishina wa Uhifadhi Tanapa, Dakta Allan Kijazi kwa ushirikiano mkubwa ambao jeshi lake la kupambana na ujangili limekuwa likitoa.
katika tukio lingine jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata majangili sugu na hatari wakiwa na nyara za serikali May 30 mwaka huu katika kitongoji cha Maji ya Chai tarafa ya King’ori wilayani Arumeru .
Amesema majangili hao watatu ambao majina yao yamehifadhiwa baada ya kuhojiwa wamekiri kuhusika kujihusisha na biashara hiyo ya ujangili.
Amesema majangili hao wamekamatwa wakiwa na vipande vine vya meno ya Tembo walivyokuwa wamefihifadhi kwenye mfuko wa Sandarusi .
Katika tukio lingine jeshi la polisi limefanikiwa kukamata watuhumiwa watatu wa wizi wa pikipiki ambao amewataja kuwa ni Hamis Juma (37) mkazi wa Olmatejoo jijini Arusha, Isiaka Islam (22) mkazi wa Majengo mkoani Kilimanjarona Hassan Mushi (54) mkazi wa Majengo mkoani Kilimanjaro.
Katika hatua nyingine jeshi la polisi linamfikisha mahakamani jambazi Jumanne Mjusi ambae alikamatwa wiki iliyopita akwa na bastola baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda, Shana ,amewaonya wananchi mkoani Arusha wanaojihusisha na uhalifu wa aina yeyote kuacha mara moja vinginevyo watatiwa mbaloni bila kujali rangi, jinsia,dini wadhifa alionao mhusika.