BARAZA la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea wameipongeza bajeti ya wakala wa barabara za vijijini na mijini Tanzania (TARURA) ya Matengenezo ya 2023/2024 ya sh billioni 2.642 na rasimu ya mpango wa bajeti ya mwaka 2024/2025.
Wakizungumza kwenye Baraza la hilo, madiwani walisema kuwa uongozi wa TARURA wilaya ya Nachingwea wanafanya kazi kubwa ya kiutendaji ukilinganisha na bajeti wanayopewa kutoka makao makuu ya TARURA.
Walisema kuwa kiasi cha fedha ambacho kimekuwa kinatengwa kwa ajili ya Matengenezo na ujenzi wa barabara katika wilaya ya Nachingwea hakiwezi kukidhi matakwa ya ukubwa wa barabara za wilaya ya Nachingwea.
Hivyo waliomba TARURA makao makuu kuwaongezea bajeti TARURA wilaya ya Nachingwea ili waweze kujenga na kufanya Matengenezo ya barabara za wilaya ya Nachingwea kurahisisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Awali akisoma taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Matengenezo ya barabara/Makalavati/madaraka na mifereji ya maji ya mvua kwa mwaka fedha 2024/2025 kwenye Baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea,Eng John Masika alisema kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 2.642.
Eng Masika alisema kuwa fedha hizo zilikuwa za mfuko wa barabara (road fund) shilingi Milioni 942.573,fedha za maendeleo ya barabara na ushirikishaji na ufunguaji wa fursa za kijamii na uchumi Milioni 200.310, fedha za Jimbo Milioni 500 na fedha za tozo ya mafuta shilingi bilioni 1 ambayo inaleta kuwa jumla ya fedha zote kuwa sh billioni 2.642.
Alisema kuwa TARURA wilaya ya Nachingwea imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 2.942 kutoka katika fedha za Matengenezo za mfuko wa barabara,fedha za maendeleo, fedha za Jimbo na fedha za tozo ya mafuta kulingana na ukomo wa bajeti uliotolewa kwa ajili ya Matengenezo ya barabara mbalimbali.