Na. Leah Mabalwe, DODOMA MAKULU
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri amewataka wazazi kutowaficha watoto wenye uhitaji maalumu na badala yake kuwapeleka shule kwa sababu nao wanatakiwa kupata elimu iliyo bora.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akiongea na Jumuiya ya Shule ya Msingi Dodoma Viziwi alipofanya ziara ya kawaida kutembelea shule hiyo iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alhaji Shekimweri alisema kuwa kila mzazi anatakiwa kumpeleka mtoto wake shule hata kama anaulemavu kwasababu ni haki yake ya msingi. “Nitoe kauli hii kwa wazazi wote, kila mtoto asiachwe nyuma, kila mtoto ananafasi ya kupata elimu na sio elimu tu na baadae kuweza kuitumikia nchi katika nafasi mbalimbali. Wazazi wote wasifiche watotot wao wenye changamoto wakakosa nafasi ya kusoma, sio tu mnakuwa hamuwatendei haki watoto bali hamjitendei haki nyie kama wazazi. Wapo wazazi ambao wanawaficha watoto wao wenye ulemavu na kuwapendelea wasio kuwa na changamoto hizo, msifanye hivyo, kwa sababu hakuna ajuae mpango wa Mwenyezi Mungu” alisema Alhaji Shekimweri.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wanafunzi wa shule hiyo kuendelea kuwa na nidhamu na kufuata taratibu zilizowekwa na kuwasikiliza wanaosimamia taaluma. “Na niendelee kuwaomba wanafunzi wote wanaosoma katika shule hii kuendelea kuwa na nizamu, kuendelea kufuata taratibu za kuishi kwenye maeneo rasmi kama hapa, kuendelea kuwasikiliza wanao simamia taaluma pamoja na nidhamu na wanafanya haya yote kwa manufaa yenu ninyi wenyewe, manufaa ya nchi yetu na manufaa ya wazazi wenu. Nawaomba muwe na nidhamu na msome kwa bidii na kila mmoja aweke malengo makubwa na mwisho wasiku kuyafikia malengo yake’’ alisema Alhaji Shekimweri.
Mkuu wa wilaya aliwashukuru walimu wote wa Shule ya Msingi Dodoma Viziwi kwa kuwa na moyo wa kujitoa kwaajili ya watoto wenye uhitaji maalumu. “Nawashukuru sana walimu wote mnaofundisha katika shule hii, tunawashukuru sana kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya. Mimi naamini kukaa na watoto wa namna hii inabidi uwe na moyo wa upendo na kujitoa sana, mnafanya kazi nzuri sana na nazidi kuwaombea muwe na moyo huohuo wa upendo kwa watoto na Mwenyezi Mungu atawabariki sana” alisisitiza Alhaji Shekimweri.
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma Viziwi, Mwl. Awadhi Mbogo akiwasilisha taarifa ya shule ya shule hiyo kwa mkuu wa wilaya alisema kuwa shule hiyo ilipanga kuandikisha wanafunzi 12 wa elimu awali na wanafunzi 24 wa darasa la kwanza. “Mpaka sasa tumeandikisha wavulana saba na wasichana sita jumla 13 kwa darasa la kwanza na darasa la awali wavulana watano na wasichana wanne jumla tisa. Hivyo, kufanya jumla ya walioandikishwa mwaka 2024 kuwa 22 kati ya 34 ya lengo sawa na asilimia 61. Tunaendelea kutoa elimu katika jamii kwa kutembelea shule na mitaa mbalimbali ili kuhakikisha tunafikia lengo la uandikishaji kwa asilimia 100” alisema Mwl. Mbogo.
Shule ya Msingi Dodoma Viziwi ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na jumla ya wanafunzi watano lengo likiwa ni kutoa fursa ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu (viziwi).