Na Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
UONGOZI bora ni nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo. Ndiyo maana Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, enzi za uhai wake aliwahi kusema, ili nchi ipate maendeleo inahitaji kuwa na vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Vitu hivi vinne kwa pamoja vikitumika ipasavyo, vinakuwa nyenzo madhubuti ya kuchechemua maendeleo kwa ustawi wa maisha ya watu na nchi yao.
Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amedhirisha kwamba ni kiongozi bora ambaye anafanya juhudi kubwa kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua za kimaendeleo kwa kuleta umoja na mshikamano nchini.
Kwa kuzingatia kuwa ujenzi wa taifa unahitaji mchango wa kila mwananchi bila kujali tofauti za kisiasa, dini, jinsi, ukanda, Rais Samia amekuwa akisisitiza na kuishi maneno yake ya kuhimiza umoja wa kitaifa ili kila mwananchi ashiriki kwa uhuru katika ujenzi wa nchi yake kupitia maarifa, mawazo, elimu na shughuli za kiuchumi anazofanya.
Moja ya falsafa aliyoiasisi Rais Samia katika ujenzi wa nchi yetu ni kuja na ‘R’ zipatazo nne (4R). Hizi ni kifupisho cha maneno ya Kiingereza Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuiding (Kujenga upya).
Maridhiano (Reconciliation) ni kitu muhimu katika ujenzi wa taifa ili kuwa na sauti moja. Rais Samia anaamini maridhiano na maelewano yanawezekana kwa kukaa pamoja na kujadiliana kwa njia ya mazungumzo na ya amani.
Palipo na maridhiano kuna maelewano, palipo na maelewano kuna amani na hivyo kuna kusonga mbele kimaendeleo. Maridhiano yanachagiza usuluhishi wa tofauti za kisiasa ili kushirikiana kwa pamoja kujenga Mama Tanzania.
Mathalani, Rais Samia ameshiriki kukaa meza moja na viongozi wa vyama vya upinzani ili kuwa na maridhiano yaliyolenga kutibu majeraha ya kisiasa na hivyo kuwa na mwanzo mwingine mzuri katika kujenga umoja wa kitaifa.
Kuongoza vyema ni pamoja kuwa mstahimilivu ukishinda majaribu mbalimbali kwani Waswahili wanasema mti wenye matunda ndio hurushiwa mawe na pia wanasema uongozi au ukubwa ni jalala. Kila mtu hutupa takataka zake hapo!
Kwa hiyo utaona ustahimilivu (Resilience) katika nchi utawezesha nchi kusonga mbele kimaendeleo. Uongozi wenye ustahimilivu utaweza kuvumilia changamoto na kukabiliana nazo ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi wake.
Viongozi hawapaswi kuyumba wanapokumbana na changamoto bali wanapaswa kusimama kwenye nafasi zao na kushirikiana na wengine kuhakikisha changamoto zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili wananchi wapate maendeleo.
Mabadiliko/Mageuzi (Reforms) hayaepukiki katika ujenzi wa nchi kwani kuleta maendeleo endelevu kunahusisha mageuzi.
Serikai ya Samia imeweka msukumo mkubwa katika kuleta mageuzi makubwa katika kila nyanja ikiwemo mageuzi ya sheria, sera na kanuni mbalimbali ili kuakisi mazingira ya wakati tulionao na hivyo kufikia azma ya kupiga hatua kimaendeleo.
Mageuzi yameonekana katika sera ya elimu, sheria za uchaguzi na sheria mbalimbali katika wizara tofautitofauti yakilenga kuongeza tija na maendeleo. Mkazo katika mageuzi au mabadiliko ya sheria ni kuongeza kasi ya maendeleo kwa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha kufikia malengo na mipango ya serikali katika kuwatumikia wananchi wake.
Kujenga upya (Rebuiding) kumekuwa moja ya msisitizo mkubwa wa Rais Samia katika ujenzi wa nchi. Kazi kubwa za kimaendeleo zimefanyika katika awamu tano za watangulizi wa Rais Samia.
Kwa upande wake, Samia analo jukumu la kuacha alama katika nchi. Rais Samia anasisitiza umaliziwaji wa miradi ya maendeleo ya awamu zilizopita na kuja na miradi mipya ya maendeleo na ya kimkakati ili kupitia miradi hiyo, wananchi wapate maisha bora, ndiyo maana ya kaulimbiu yake ya “Kazi iendelee” kwani watangulizi wake wote wamekuwa na dhamira njema ya kujenga upya nchi.
Kujenga upya nchi kunahusisha kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kujenga miundombinu na uboreshwaji wa huduma za kijamii. Haya na mengine mengi mapya yanayofanyika chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia yanatimiza mwekeleo wake wa kuijenga upya nchi yetu hasa katika nyanya ya kiuchumi na kijamii.
Januari 21, 2024, Rais Samia alishiriki ibada maalumu ya kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, ibada iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Azania Front, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Katika ibada hiyo, Rais Samia alisema ili kuwe na amani na mshikamano wa kitaifa, serikali yake imekuja na falsafa ya 4R ambazo atazitumia katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Baba Askofu Malasusa, umezungumzia umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, kuhusu amani nakubaliana nawe kwa asilimia 100 kwamba tukiwa wamoja tutajenga taifa lenye nguvu. Katika uongozi huu, tumekuja na falsafa ya R4, Kiswahili chake ni maridhiano, mageuzi, ustahimilivu na kujenga upya taifa letu. Nizihusishe R4 na maneno yaliyosemwa kwenye kitabu cha Marko sura ya 3: 25 – Na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama” amesema Rais Samia.
Vilevile, Rais Samia alisisitiza kuwa 4R zitasaidia kukuza demokrasia nchini. “Si kila aliye kwenye mchakato wa demokrasia ni mwanademokrasia, wengine ni wanaharakati, kuna tofauti na haya mawili, tutaendelea kulinda misingi ya demokrasia hapa nchini kwetu inayowezesha demokrasia kushamiri zaidi,” alisema Rais Samia.
Katika kuonesha kwamba Samia anayaishi maneno na ahadi zake, Jumatano iliyopita (Januari 24), Chama Kikuu cha Upinzani nchini (CHADEMA) kilifanya maandamano kushinikiza serikali kuondoa bungeni miswada mitatu ya mabadiliko ya sheria za uchaguzi na kuboresha katiba mpya, pamoja na mambo mengine.
Kwa lugha nyingine chama hicho kinataka serikali kufuata maoni ya chama hicho katika kuboresha miswada hiyo!
Wengi walidhani serikali ingezuia maandamano hayo ya amani lakini uongozi wa serikali ya Awamu ya Sita haukuzuia abadani maandamano hayo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pamoja na viongozi wengine wa chama hicho, Godbless Lema, Benson Kigaila na Joseph Mbilinyi waliongoza msafara wa waandamanaji hao waliokuwa wameshika bendera za chama hicho na mabango yenye jumbe mbalimbali.
Jeshi la polisi lilitoa kibali cha kuwaruhusu kufanya maandamano hayo na kuahidi kuyasimamia.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya mji wa Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alifika eneo la Buguruni mapema asubuhi na kuanza kuongoza misafara ya pikipiki na magari kabla ya maandamano hayo kuanza
Kwa ujumla, maridhiano, ustahimilivu, mageuzi/mabadiliko pamoja na kujenga upya ni nyenzo muhimu ya amani, demokrasia na maendeleo nchini.
Pamoja na dhamira njema aliyonayo Rais wetu ya kutaka kuona 4R zinatekelezwa ipasavyo, viongozi wa dhima ya kutoa ushirikiano ipasavyo ili kukamilisha azma aliyonayo Rais Samia ya kutaka kuona Tanzania yenye amani, upendo, mshikamano, demokrasia na maendeleo. Hii inawezekana kwa kuitendea haki falsafa ya 4R kwa vitendo.
Dk. Reubeni Michael Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa-Dodoma. Maoni: 0620 – 800 462.