Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Mkoa wa Mwanza mara baada ya uzinduzi wa ugawaji wa Boti za Kisasa na vizimba kwa ajili ya Wavuvi wa Kanda ya Ziwa katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza tarehe 30 Januari, 2024.
……………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Mikoa ya Kanda ya ziwa kuhakikisha wanawasimamia wavuvi waliopewa Boti na Vizimba ili wazitumie zana hizo kwa matumizi sahihi yatakayosaidia kupunguza uvuvi haramu nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Januari 30, 2024 Jijini Mwanza kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa Vizimba 222 vya kufugia samaki na Boti za kisasa 55 kwa wavuvi Kanda ya ziwa.
Amesema kunaumuhimu mkubwa wa kufatilia kwa ukaribu maendeleo ya walionufaika sanjari na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya zana hizo ili kusaidia ukuaji wa Sekta ya uvuvi.
Ameeleza kuwa shughuli zote za uvuvi nchini lazima ziendeshwe kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili rasilimali za uvuvi ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.
“Uchomaji wa nyavu na zana za uvuvi kwa lengo la kukabiliana na uvuvi haramu unarudisha sana nyuma maendeleo ya wavuvi pia inajenga chuki kati ya wavuvi na Serikali,tunachokifanya sasa kwenye utoaji wa vifaa vya kisasa ninahakika nyavu zilizotolewa siyo za makokolo ni nyavu salama hivyo niwaombe Wizara ya Mifugo na Uvuvi muongeze kasi katika kusambaza nyavu hizo ili wavuvi waachane na nyavu haramu” Amesema Rais Samia
Kwaupande Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema, kutokana na uhitaji wa watanzania wa kuwa na zana za kisasa wamezamilia kuweka boti zisizo pungua 800 nchini zitakazo wafaa wavuvi.
Amesema zana zilizotolewa kwa wavuvi zitawawezesha kufikia malengo ya ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020,mpango watatu wa maendeleo ya miaka mitano 2021 hadi 2025 sera ya Taifa ya uvuvi ya mwaka 2015 na mpango kabambe wa uvuvi wa mwaka 2022,2023,2036 na 2037.
Aidha, ameeleza kuwa kutokana na maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika katika Sekta hiyo yatasaidia kuongeza pato la Taifa kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 10 pia wataongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi kwa asilimia 35 kutoka kwenye uzalishaji wa sasa ambao ni tani laki tano hadi laki saba.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amesema, kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2018,2022 unaonesha samaki katika ziwa Victoria wamepungua kwa asilimia 30.
“Tulikuwa na viwanda 15 lakini vinavyofaya kazi ni viwanda 8 hadi sasa tumeathiriwa na uvuvi haramu,Mkoa umeshachukua hatua mbalimbali na kuweka mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu ili tuweze kuwa na uvuvi endelevu”, Amesema Makalla.
Kilisanti mtenya ni miongoni mwa wanufaika wa zana za uvuvi ameiomba Serikali ijenge viwanda vya kuchakata chakula cha samaki katika Mikoa ya Kanda ya ziwa ili kurahisisha upatikanaji wa chakula hicho kwa bei nafuu