Na Sophia kingimali
Kufuatia uhaba wa wahandisi wanawake katika fani hiyo SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limezindua programu maalum inayolenga kuwajengea uwezo wahandisi wanawake, kuwaendeleza kiujuzi na kielimu,kwa lengo la kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uendelezaji miradi ya umeme nchini.
Akizungumza leo januari 29,2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gisima Nyamo_Hanga amesema,programu hiyo ni ya miaka minne na watashirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT),ambavyo watavitumia kuwaendeleza kielimu wataalamu wakike washirika hilo, na kuwapata wanafunzi wanaohitimu fani ya uhandisi.
“Ushiriki wa wahandisi wanawake bado ni mdogo hususani katika sekta ya umeme,na sisi kama TANESCO tumeona ni muhimu kuja na mkakati maalum ambao utasaidia kuongeza wahandisi wengi wa kike ambao tutawaajiri na kufanya nao kazi.
“Mradi huu unaratibiwa na Umoja wa Ulaya, lakini mpango wetu wa mbele ni kuhakikisha kwamba unakua endelevu na hata baada ya huu mradi kuisha sisi wenyewe tuweze kuendelea, lengo ni kuwapata wahandisi wengi wakike wengi,”amesema.
Ameongeza kuwa, mradi huo umeanza na wanawake 40 ambao wanawezeshwa kielimu katika vyuo vikuu vya ndani na programu hiyo itakua ni ya miaka minne.
Aidha Mhandisi Nyamo_Hanga ametoa rai kwa wahandisi wakike kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika mpango huo.
“Mradi huo ni moja ya kichocheo cha kuwahamasisha watoto wakike kusoma fani ya uhandisi, mradi huu tumeanza na wanawake 40 lakini kila mwaka tutakua tunaongeza wengine,”amesema.
Kwaupande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dk. Seif Shekalage, amesema programu hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wanawake wanaendelezwa kiuchumi, kielimu na kuongeza usawa wa kijinsia.
Amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maluum ipo tayari kushirikiana na TANESCO ili programu hiyo iwe mfano bora na wa kuigwa na taasisi na mashirika mengine nchini.
“Serikali itaendelea kushirikiana na TANESCO ili kuhakikisha idadi ya wanawake katika shirika inaongezeka mpaka kufikia 2026″Amesema Shekalage.
Naye mnufaika wa programu hiyo Mhandisi Catherine Mwigoha kutoka TANESCO,amesema kupitia mradi huo utasaidia kuwaongezea ujuzi,ambao utawezesha kuongezeka kwa uzalisaji ndani ya shirika hilo.
Ameongeza kuwa mradi huo utawasaidia kupata fursa ya kushika nafasi mbalimbali za maamuzi na kuongeza uzoefu wa kupata nafasi za ajira.