WANANCHI wa kata ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea wamefanikiwa kuchimbiwa visima virefu vinne vya maji safi na salama kutokana na kufikisha kero ya ukosefu wa maji kwa miaka mingi.
Akizungumza wakati uchimbaji wa kisima katika Kijiji cha Kilimarondo kata ya Kilimarondo, Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa alipokea kero ya wananchi kukosa maji Kwa muda mrefu ndipo akaiwakilisha kwa mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Mkoa akaongea na waziri Juma Aweso ndio maana wamefanikiwa kuchimbiwa visima virefu vya maji.
Moyo alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia suluhu Hassan inafanya kazi kwa vitendo hivyo dhamira ya dhati ya Rais Dr Samia kumtua mama ndoo kichwani inatimia kwa vitendo na wananchi wanaona matokeo yake.
Alisema kuwa vikikamilika visima vinne virefu vya maji katika kata ya Kilimarondo basi eneo hilo tatizo la maji litakuwa limekaishwa kabisa na wataanza kutatua changamoto nyingine zilibaki ambazo wananchi bado hawajatatuliwa.
Moyo alisema kuwa anamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa jitihada alizozifanya za kusaidia kupatikana kwa njia sahihi ya kutatua kero ya maji katika kata ya Kilimarondo.
Awali akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kilimarondo kata ya Kilimarondo,waziri wa maji Juma Aweso alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dr Samia suluhu Hassan inania ya dhati kuhakikisha inatatua kero ya maji na kufanikiwa kumtua mama ndoo kichwani.
Aweso alisema kuwa serikali ya awamu ya sita umenunua gari la kujimbia visima kila Mkoa hivyo viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza wahakikishe wanachimba visima vya kutosha ili kumaliza kero ya wananchi ya kukosa maji kwa miaka mingi.
Alimalizia kwa kuuagiza uongozi wa RUWASA Mkoa wa Lindi kuhakikisha wananchi visima virefu vya maji safi na salama katika vijiji vyote vya kata ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Nao baadhi wananchi wa Kijiji cha Kilimarondo kata ya Kilimarondo wamemshukuru mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo kwa kufikisha kero ya ukosefu wa maji safi na salama na kufanikiwa kutatuliwa kero hiyo kwa muda mfupi sana.