Dar es Salaam
Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) nchini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff wakati wa kikao cha pamoja cha Menejimenti ya Wakala huo na Mameneja wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika kwenye ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Seff alisema kufanya kazi kwa weledi itasaidia kukamilisha majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi na hivyo kuonesha kwamba wanaweza kwani watakua wamefanya kazi kama inavyotakiwa.
Aidha, Mhandisi Seff amewataka Mameneja hao katika kipindi hiki cha msimu wa mvua nyingi hususan inapotokea dharura waweke alama ambazo zitamuonesha mwananchi kwamba eneo fulani halipitiki na ili kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza.
Hata hivyo Mhandisi Seff amewapongeza Mameneja hao kwa kazi kubwa wanazofanya katika maeneo yao ya kazi kwa kuendelea kuwahudumia wananchi.
Kuhusu maadili ya wafanyakazi wa TARURA , Mkurugenzi wa huduma Saidizi wa wakala huo Bi Azimina Mbilinyi alitumia kikao hicho kuwakumbusha viongozi na watumishi wote kwaujumla kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia misingi na kanuni za utumishi wa umma kwani zipo wazi na zinafahamika.