Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan akiangalia bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na kiwanda cha INDESSO cha jijini Jakarta kinachochakata majani ya karafuu na kuzalisha mafuta kwa matumizi mbalimbali. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake wakiwa katika kigari maalum walipotembelea Makao Makuu ya Kiwanda cha INDESSO kinachochakata majani ya karafuu na kutengeneza mafuta kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan tarehe 26 Januari, 2024 ametembelea Makao Makuu ya Kiwanda cha INDESSO kinachochakata majani ya karafuu na kutengeneza mafuta kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Katika ziara hiyo kwenye kiwanda cha INDESSO ambacho kimewekeza kisiwani Pemba, Mhe. Rais Samia alijionea mchakato mzima wa uchakataji majani ya Karafuu na kutengeneza mafuta kupitia vinu vitano vilivyopo kwenye kiwanda hicho.
Akizungumza mbele ya Mhe. Rais Samia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Indesso, Bw. Robby Gunawan alisema Indesso inajivunia mafanikio mbalimbali iliyofikia ikiwemo kuwa kichocheo cha mabadiliko katika tasnia ya karafuu ya Tanzania”.
“Kwa kuwekeza katika eneo hili, hatujafungua tu fursa za ukuaji wa kiuchumi bali pia tunachangia katika maendeleo endelevu ya jamii za wenyeji,” alisema.
Aliongeza kuwa biashara ya kuchemsha mafuta ya majani ya karafuu bado iko katika hatua za awali za maendeleo nchini Tanzania na inaweza kuwa njia ya kusukuma ukuaji wa kiuchumi na maendeleo vijijini.
Alisema Indesso ina matumaini kuwa mipango yao itakuwa kichocheo, kuhamasisha watu kuanzisha vituo zaidi vya kuchemsha mafuta ya karafuu ndani ya Tanzania.
Katika ziara hiyo, Mhe. Rais aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mhe. Mudrick Ramadhan Soragha, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Makocha Tembele na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jat Miko.
Mhe. Rais Dkt. Samia na ujumbe wake wameondoka Indonesia kurejea nchini baada ya kumaliza ziara ya kitaifa ya siku tatu iliyofanyika nchini humo kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024.