Mtendaji Mkuu wa DART Dkt. Athumani Kihamia akizungumza na watumishi wa Wakala huo 26/1/2024 katika ofisi za DART Ubungo maji Jijini Dar es Salaam
………………………………..
Na. Martha Komba.
Watumishi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, uadilifu uaminifu na kujituma zaidi ili kuongeza tija katika mradi wa DART. .
Maelekezo hayo yametolewa Januari 26, 2024 katika Ofisi za Wakala huo Ubungo Maji Jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa DART Dkt. Athumani Kihamia alipokutana na watumishi wa Wakala kwa lengo la kufahamiana na kuelekezana mikakati ya kuendelea kutoa huduma bora ya usafiri wa umma kwa watanzania.
“Tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa weledi, uadilifu na uaminifu muda wote tunapokuwa kazini, pia tuzingatie maadili ya utumishi wa umma hasa suala la kutunza Siri za Serikali ambalo ni jukumu la kila mmoja wetu” Alisema Dkt..Kihamia.
Dkt.Kihamia ameongeza kuwa ni vyema kila mtumishi kufanya kazi kwa mpangilio ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango kazi wa siku, wiki na mwezi jambo ambalo litasaidia kupata mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya kila mmoja samamba na kutatua changamoto zinazoweka kujitokeza.
“Ninaposema kufanya kazi kwa mpangailio ninamaanisha kuwa na mpango kazi wa siku, wiki na miezi kwa kila mtumishi wa DART kwani kufanya kazi bila kuwa na dira ambayo ndio huo mpangokazi ni sawasawa na chombo kinachojiendesha bila kuwa na mwelekeo”. Alisema Dkt..Kihamia.
Aidha, Mtendaji Mkuu alisisitiza wakuu wa idara na vitengo kuwa na uelewa wa Pamoja katika mipango kazi watakayoandaa ili isitokee kwamba mpango unajulikana na ngazi za juu pekee bila watumishi wa chini kuufahamu, akitolea mfano mpango wa mafunzo kwa watumishi ambao kila mtumishi katika idara anatakiwa kuufahamu ili inapotokea nafasi ya mtumishi Kwenda kusoma isionekane kuwa amependelewa bali ni kwa mujibu wa mpango.
Dkt. Kihamia pia aliwataka watumishi kudumisha upendo na kuepuka tabia za majungu ambazo hazileti tija katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku mahala pa kazi.
Mtendaji Mkuu alitumia kikao hicho kupata changamoto mbali mbali zinazoukabili mradi na namna ya kuzitatua ikiwemo suala la uhaba wa Mabasi, kutokuwa na mageti na kadi janja, suala la lugha mbaya na isiyo na staha kwa watumishi Pamoja na tatizo la kukatika kwa umeme ambali linaathiri utoaji wa huduma vituoni.
Dkt. Kihamia ameteuliwa hivi karibuni na Mh. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mtendaji Mkuu Dkt.Edwin Mhede.