OR-TAMISEMI
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi ametembelea na kuzindua majaribio ya mfumo wa ufundishaji mubashara “Live Teaching” ambao utawezesha wanafunzi wa shule nyingine nchini kuunganishwa na mwalimu anayefundisha katika shule ya Sekondari Kibaha ili kupunguza uhaba walimu nchini.
Akizungumza mara baada ya kujionea majaribio ya mfumo huo ambapo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma walikuwa wameunganishwa na mwalimu anayefundisha Kibaha Sekondari, Mhe. Ndejembi amesema hatua hiyo ni jitihada kubwa ya kukuza elimu inayofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
“ Niwapongeze sana Shirika la Elimu Kibaha kwa kuja na mfumo huu ambao unasimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, hizi zote ni jitihada kubwa zinazofanywa na Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kiwango cha elimu kinakua kwa kukabiliana na changamoto hii ya uhaba wa walimu nchini.”
“Kwahiyo nitoe rai kwenu kuhakikisha mfumo huu unafanya kazi kama ilivyokusudiwa na wanafunzi wetu nchini wananufaika na matunda haya makubwa yanayofanywa na Rais wao,” amesema Mhe. Ndejembi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Ndejembi na kwamba watahakikisha mfumo huo unasambaa kwa kasi nchini ili kila shule iweze kunufaika nao.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Elimu kutoka Shirika la Elimu Kibaha, Dkt. Rodgers Shemwelekwa amesema “Kwa kiasi kikubwa sana mfumo huu utaenda kuondoa changamoto ya uhaba wa walimu kwahiyo yale maeneo yenye uhaba wa walimu sasa wanafunzi wake watakuwa wanaunganishwa na wenzao watakaokuwa wanafundishwa kutokea Shule ya Sekondari Kibaha,” amesema Dkt.Shemwelekwa.
Baada ya majaribio ya leo katika Shule ya Sekondari Dodoma mfumo utaenda katika Shule 10 na baadaye utasambazwa katika Shule zote nchini.