Afisa mtendaji wa Kata ya Kitangiri Stella Kilawe akitoa elimu ya usafi wa mazingira kwa wafanyabiashara
Mwenyekiti wa wafanyabiashara, masoko na minada Mkoani Mwanza Justine Sagara akizungumza kwenye kikao cha elimu ya usafi wa mazingira kilichofanyika kwenye mnada wa Kitangiri uliopo Wilaya ya Ilemela Mkoani mwanza
……………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wafanyabiashara wadogo maarufu (machinga)Mkoani Mwanza wameiomba Serikali kuboresha mazingira ya minada na kuwajengea vyoo ili waweze kufanya kazi zao kwenye mazingira rafiki.
Ombi hilo limetolewa leo Alhamisi Januari 25, 2024 na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara,masoko na minada Mkoani humo Jastine Sagara wakati akizungumza kwenye kikao cha utoaji wa elimu ya usafi wa mazingira kilichofanyika kwenye mnada wa Kitangiri uliopo Wilaya ya Ilemela Mkoani mwanza.
Sagara ameeleza kuwa mnada wa Kitangiri ni miongoni mwa mnada kongwe lakini tangu wameanza kufanya biashara hakuna huduma ya choo hivyo wafanyabiashara kulazimika kwenda kujisaidia kwenye nyumba ya mtu binafsi.
“Siku akisafiri au wafanyabiashara wakimuudhi na akaamua kufunga choo chake tutakosa sehemu ya kujistri hivyo mazingira yetu yatachafuka kutokana nawatu kujisaidia hovyo tunaiomba Serikali itujengee choo ili tuwe na huduma hiyo ya kudumu”, Amesema Sagara
Amesema katika kipindi hiki cha mlipuko wa kipindupindu Serikali inahimiza suala la usafi kwenye masoko,minada pamoja na utoaji elimu hivyo wanapaswa kuwawekea miundo mbinu rafiki ili waweze kuepukana na magonjwa hayo ikiwemo Kipindupindu.
Baadhi ya wafanyabiashara wameeleza kuwa licha ya wao kuwa sehemu ya wachangiaji katika pato la Taifa bado miundombinu katika maeneo yao ya kazi hususani choo imekuwa changamoto hali inayopelekea kushindwa kufanya shughuli zao kwa amani.
“Tunawaomba viongozi wa Serikali waliopata dhamana kuweka utaratibu wa kutembelea katika maeneo ya minada ili kuweza kuona na kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili” Wamesema
Akijibu suala la ukosefu wa miundombinu ya choo katika mnada huo Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Kitangiri Stella Kilawe, amesema kutokana na kero ya ukosefu wa choo tayari swala hilo wameweza kulifikisha katika vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) kwa ajili ya kuweka msisitizo wa kuboreshewa mnada ili uwe katika hali ya usafi.
“Nimuombe mweshimiwa Diwani aende akaongee na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya choo,hivyo tunaomba muendelee kuwa wavumilivu wakati suala hili linatafutiwa ufumbuzi”Amesema Kilawe.