Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akizungumza na wananchi wa Amani Makoro mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kitai-Lihuli, sehemu ya Amani Makoro – Ruanda (km 35), kwa kiwango cha lami, Mkoani Ruvuma.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group anayejenga barabara ya Kitai-Lihuli, sehemu ya Amani Makoro – Ruanda (km 35), Mkoani Ruvuma.
Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara ya Kitai-Lihuli, sehemu ya Amani Makoro – Ruanda (km 35), kwa kiwango cha lami, Mkoani Ruvuma.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kitai-Lihuli, sehemu ya Amani Makoro – Ruanda (km 35), inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Ruvuma.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa Mhandisi Mshauri LEA Associaties anayesimamia ujenzi wa barabara ya Kitai – Lituhi sehemu ya Amani Makoro-Ruanda (km 35) kwa kiwango cha lami na kuutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuendelea kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika.
Pia, ameagiza Mkandarasi anayejenga barabara hiyo China Railway Seventh Group kutopewa miradi mipya mpaka hapo atakapokamilisha miradi aliyopewa katika mkoa wa Mara, Katavi ambayo nayo inaonekana kusuasua.
Bashungwa ametoa agizo hilo leo tarehe 25 Januari 2024 wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo ambapo hajaridhishwa na utekelezaji wake ambao umechelewa kwa asilimia 75 na kusisitiza hatua za kimkataba zichukuliwe dhidi ya Mhandisi Mshauri huyo.
“Nimuagize Katibu Mkuu kuangalia hatua za kimkataba mnazotakiwa kumchukulia haraka Mhandisi Mshauri kwasababu ameshindwa kumsimamia Mkandarasi kukamilisha mradi huu kwa wakati”,amesisitiza Waziri Bashungwa.
Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishatoa Bilioni 6.9 ambayo imekamilisha kipande cha kwanza cha kilometa 5 kutoka Kitai hadi Amani Makoro na Bilioni 60 kwa ajili ya muendelezo wa barabara hiyo sehemu ya Amani Makoro – Ruanda.
“Kiasi cha Shilingi Bilioni 155 zimetengwa ajili ya mradi mzima wa ujenzi wa barabara kuanzia Kitai – Lihuli – Bandari ya Ndumbi”, amefafanua Bashungwa.
Bashungwa ameagiza TANROADS kutoendelea kulimbikiza miradi kwa Wakandarasi kwani ndiyo inafanya miradi mingi kuchelewa na mingine ikiwa ya kimkakati na kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, amesema kuwa maendeleo ya mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 25 ikilinganishwa na asilimia 100 ambapo mradi huo ulitakiwa kukamilika Disemba, 2023.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma , Kanali Labani Thomas, amesema kuwa Mchuchuma na Liganga wanaitegemea barabara hii kwani ndio barabara muhimu na ni kiunganishi cha kutoka Mkoa wa Ruvuma kupitia Nyasa kwenda mkoani Njombe kupitia Ludewa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Ruvuma, Komred Oddo Mwisho, amesema kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kati ya Wilaya ya Nyasa-Mbinga kwani ndipo uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe yanapofanyika na kwa siku takribani magari 400 hadi 500 yanapita katika barabara hiyo kuyasafirisha kuelekea maeneo mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Mhe. Benaya kapinga, amesema kuwa kilio kikubwa cha Wananchi wa Amani – makoro hadi Ruanda ni kupata barabara kwa kiwango cha lami ili kuchochea maendeleo ya wananchi.
Waziri Bashungwa yupo mkoani Ruvuma katika ziara yake ya kikazi ambapo atakagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.