Na Sophia Kingimali
Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzani (DCEA) imemkamata kinara wa mtandaoa wa wafanyabiashara wa dawa ya kulevya aina ya Cocaine pamoja na kukamata kilo gramu 692,336 za dawa hizo na watuhumiwa wengine wa nne.
Taarifa hiyo ameitoa kamishna Jenerali Aretas Lyimo leo januari 25,2024 jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kinara huyo alikua akitafutwa muda mrefu na amefanikiwa kukamatwa maeneo ya Boko wilaya ya Kinondoni na wenzie watatu huku mmoja akikamatwa wilaya ya Mbeya mkoa wa Mbeya kijiji cha Shamwego.
“Huyu mfanyabiashara ni mkubwa kwa wiki anauwezo wa kusafirisha watu 10(punda)kwa ajili ya kusambaza dawa hizo maeneo mbalimbali Duniani kibaya zaidi anatumia watoto wa maskini kuwabebesha dawa hizo na hatimae wengine wanafia njiani”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Aidha kamishna Lyimo amefafanua kuwa dawa hizo aina ya Cocaine huzalishwa kwa wingi katika bara la Amerika kusini na kusafirishwa kwa njia ya Anga na wabebaji ni Punda.
Amesema dawa hizo wanazimeza kwa mfumo wa pipi ambapo mtu mmoja anabeba kilogramu 300 mpaka 1200 na wengine hubeba hadi gramu 2000 kwa wakati mmoja.
“Huyu mfanyabiashara tuliyemkamata ana mtandao mkubwa wa wabebaji(punda) kutoka nchi mbalimbali hivyo makosa yake yanaangukia katika uharifu wa kupangwa unaovuka mipaka”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Sambamba na hayo kamishna Lyimo ametangaza operesheni kali mwaka huu 2024 ya kupambana na dawa za kulevya ambapo itafanyika nchi kavu na baharini.
Amesema kwa nchi kavu Oparesheni hiyo itahusisha mashamba ya dawa hizo,mipaka na kwenye maeneo yote yakusambazia ikiwemo vijiwe vya usambaji na watumiaji.
Akizungumzia Oparesheni baharini amesema itahusisha fukwe na katikati ya bahari lakini pia kwenye maeneo yote yanayouza shisha.