Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amekagua ujenzi wa mradi wa barabara kwa kiwango cha Lami wenye urefu wa km 36.2 wenye thamani ya bil 69 unaotekelezwa katika kipindi cha muda wa miezi 36 kutoka Kitulo hadi Iniho wilayani Makete Mkoani Njombe.
Akizungumza mara baada ya kukagua kambi ya mkandarasi na barabara ambayo imeanza kusafishwa tayari kwa kuanza ujenzi Bashungwa amemtaka mkandarasi wa kampuni ya kichina ya China National Aero Technology International Enginnering Corporation CNATIEC kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo kwasababu ya uhitsji mkubwa wa wananchi kwa ajili ya kusafirisha mazao na kuunganisha na mkoa wa Mbeya huku pia akiagiza kutekeleza matakwa yote ya mkataba.
Kuhusu fidia ya barabara ya Njombe Makete yenye urefu wa km 107 ambayo imekamilika ,Waziri amesema rais ametoa maelekezo kwa wizara ya ujenzi kupeleka mil 622 kwa ajili ya kulipa fidia kwa watu wote ambayo walikuwa hawajalipwa kwa kupisha mradi huo.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mhandisi Jephason Nko ambaye ni kaimu mkurugenzi wa miradi TANROADS amesema hadi sasa mradi huo umefika asilimia 4.2 badala ya 8.2 hivyo wataongeza usimamizi kwa mkandarasi na ufatiliaji ili aweze kuendelea na ujenzi hata kipindi hiki cha mvua kwa kazi ambazo haziathiriwi na mvua zinazoendelea.
“Mradi huu ulianza kutekelezwa miezi sita iliyopita hivyo upo nyumba kimkataba ,lakini sababu kubwa ni mvua kubwa zinazoendlea lakini nikuhakikishie mh waziri kumsimamia mkandarasi ili aongeze kasi na kufanya ujenzi kwa baadhi ya kazi hata kipindi cha mvua”alisema Mhandisi Jephason Nko .
Mara baada ya kupokea maagizo ya serikali kwa niaba ya mkurugenzi wa Kampuni mhandisi Cui Aifu akasema wamepokea maelekezo ya kuongeza rasilimali watu,watalaamu na mitambo ili kuifanya kazi kwa wakati na kumaliza ndani ya muda wa mkataba.
Kwa upande wake mbunge wa Makete Festo Sanga ameishukuru serikali kwa kutoa fedha nyingi kutekeleza mradi miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa Ngano,Pareto na barabara ikiwemo ya Huo wa Kitulo -Iniho Utakaogharimu zadi ya bil 69 ambao ni muhimu sana kwa wakazi wa wilaya hiyo inayozalisha mazao mengi ya biashara hususani viazi.
Hamasa ya kuboresha miundombinu ya barabara Njombe Inakuja kutokana na Uzalishaji Mkubwa wa mazao ya Biashara lakini licha ya uwingi wa chakula ila mkoa huo unakabiliwa na tatizo kubwa la udumavu jambo ambalo limemsukuma mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka kuja na Kampeni ya kutokomeza udumavu yenye kauli mbiu isemayo “Kujaza tumbo sio lishe ,Jali unachomlisha” ambayo imeungwa mkono na Waziri Bashungwa ambaye amewataka wakazi wa Njombe kutumia vyakula wanavyozalisha kwa chalula badala ya kujikita kwenye biashara ili kuwa na kizazi kisicho na changamoto ya udumavu,Utapiamlo na Ukondefu.